Rais Donald Trump amemfuta kazi Waziri wa Ulinzi Mark Esper, na kutangaza kwenye Twitter kwamba afisa huyo wa ngazi ya juu wa Marekani "amefutwa".
Christopher Miller, mkuu wa sasa wa Kituo Cha Kukabiliana na ugaidi amechukua nafasi hiyo mara moja.
Hii ni baada ya wawili hao kutofautiana hadharani katika wiki za hivi karibuni.
Bw. Trump mpaka sasa hajakubali kushindwa katika uchaguzi wa Marekani na rais mteule Joe Biden, na ameapa kupinga matokeo hayo mahakamani.
Wiki chache zilizosalia kabla ya Biden kuchukua ofisi Januari 20, Trump bado ana uwezo wa kufanya maamuzi.
Bw Miller alionekana akiingia makao makuu ya kitengo cha ulinzi Pentagon siku ya Jumatatu muda mfupi kabla ya Bw. Trump kutangaza kufutwa kwake.
Afisa huyo wa zamani wa vikosi maalum alihudumu katika baraza la usalama la kitaifa la Rais Trump kabla ya kuwa mkuu wa Kituo cha kukabilina na ugaidi mwezi Agosti.
Katika barua ya kuacha kazi, Bw Esper aliwashukuru maafisa wa vikosi vya jeshi na kusema kwamba anajivunia yale aliyoweza kufikia katika kipinďi cha miezi 18 alichohudumu Pentagon.
"Nilihudumia nchi yangu kwa mujibu wa katiba, kwa hivyo nakubali uamuzi wako wa kumleta mtu mwingine kuchukua nafasi hii ," aliandika.
Mwanasiasa wa ngazi ya juu wa Chama cha Democratic Nancy Pelosi amekosoa uamuzi huo.
"Kufutwa ghafla kwa waziri Esper ni ishara wazi kwamba Rais Trump ana lengo la kutumia siku zake za mwisho ofisini kuvuruga demokrasia ya Marekani na sehemu nyingine duniani," alisema spika huyo wa Bunge la Wawakilishi.