Fahamu: Bunge la Tanzania Liliwahi Kufanya Vikao Kwenye Jengo la Freemason



WASOMAJI kadhaa wa gazeti la UWAZI wameomba Historia ya Bunge letu ambalo limezinduliwa na Rais Dk John Magufuli Novemba 13 mwaka huu. Historia ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaanzia Machi 19, 1926 siku ambayo Bunge la Uingereza lilipisha sheria iliyoitwa The Tanganyika Legislative Council Order in Council, 1926. Baraza la Kutunga Sheria lilipata wajumbe wake wananchi kwa mara ya kwanza mwaka 1945.


 


 


Mabadiliko mengine makubwa yalifuata mwaka 1953. Baraza liliachana na mfumo wa Gavana kuwa mwenyekiti na kuanzishwa kiti cha Uspika. Spika wa kwanza wa Baraza la Kutunga sheria alikuwa Brigadia Willliam E.H Scupham, aliapishwa Novemba mwaka 1953.


 


 


Aprili 1955 wajumbe wanawake wa kwanza waliapishwa na kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. Baada ya Uchaguzi wa mwaka 1958, ulioshirikisha vyama vya TANU (Tanganyika African National Union), United TanganyikaParty (UTP), na African National Congress (ANC).


 


Wajumbe wa kuchaguliwa walipatikana kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi huo huku TANU ikifanikiwa kupata viti vyote katika uchaguzi huo na kukifanya kuwa chama cha kwanza kuingia katika LEGCO. Wakati Tanganyika inajiandaa na uhuru.


 


Agosti 30, 1960 ulifanyika uchaguzi wa pili ili kupatikana wajumbe wa kuchaguliwa kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. Baraza la Kutunga Sheria lilibadilishwa jina na kuwa Bunge (National Assembly) kupitia sheria ya Tanganyika Order in Council 1961 au pia ilikuwa inaitwa Constitution Assembly of Tanganyika 1961.


 


Spika Abdulkarimu Yusufali Alibhai Karimjee alikuwa spika tangu wakati wa ukoloni; aliendelea kuwa Spika mpaka Desemba 26,1962. Mwaka 1962 hadi 1964 mabadiliko makubwa ya kikatiba yalitokea baada ya Bunge la Tanganyika kujibadilisha na kuwa Bunge la Katiba. Moja ya mabadiliko ilikuwa sheria zote zilizopitishwa na Bunge zilisainiwa na Rais wa Tanganyika badala ya Gavana.


 


Pia Rais wa Tanganyika alikuwa na nguvu ya kulivunja Bunge. Hata baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 na hatimaye muungano wa Tanganyika uliozaa Tanzania Aprili 26, 1964, Bunge la Jamhuri liliendelea kutumia katiba ya Tanganyika kama katiba yake na pia makubaliano ya Muungano yalitumika.


 


 


Awamu nyingine ya Bunge inaonekana kuanzia mwaka 1965 ambapo chama kilishika hatamu hivyo Bunge likapungua nguvu yake na kufanya kamati kuu ya chama kuwa juu ya dola.


 


 


Katika kipindi hicho cha mpito kuanzia mwaka 1965 hadi 1977, Bunge lilikuwa linatumia katiba ya Tanganyika kama katiba ya mpito. Hata hivyo ndio wakati huo Baraza la Wawakilishi lilipoundwa Zanzibar, kuanzia hapo ukaanzishwa utaratibu wa baadhi ya Wawakilishi kutoka Baraza la wawakilishi Zanzibar kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.


 


 


Baraza la Kutunga Sheria hapo awali lilikuwa likifanya vikao vyake kwenye Ukumbi wa Anatouglou (Mnazi Mmoja Dar es Salaam). Baadaye Baraza hili lilihamishia shughuli zake katika jengo linaloitwa Freemason Hall lililopo mkabala kwa nyuma na Hyatt Hotel Kilimanjaro na linamilikiwa na Jumuiya ya Freemason. Baadaye lilihama hapo Freemason na likawa linakutana katika Ukumbi wa Karimjee mjini Dar es Salaam.


 


Kunako mwishoni mwa miaka ya 1970 na mapema miaka ya 1980 mikutano midogo ya Bunge ilianza kufanyika kwenye Ukumbi wa CCM Dodoma, huku mkutano wa Bajeti ukiendelea kufanyika Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam.


 


 


Utaratibu huu uliendelea hadi mwishoni mwa miaka ya tisini ambapo Bunge lilianza kufanya mikutano yake yote Dodoma kwenye Ukumbi wa Piu Msekwa. Kwa kuwa kumbi zote zilizotajwa hapo juu hazikuwa kumbi zilizojengwa mahususi kwa ajili ya Bunge, mwaka 2000 Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alielekeza Bunge kuwa na ukumbi wake mahususi.


 


 


Ujenzi wa Ukumbi Mpya wa Bunge ulikamilika mwaka 2006 mjini Dodoma na ndio unaotumika sasa chini ya Spika Job Ndugai. Katika mgawanyo wa madaraka nchini, Ibara ya 4 ya Katiba ya Tanzania imelipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria na kuisimamia Serikali katika utekelezaji wa shughuli za umma nchini.


 


Ili kutekeleza majukumu yake likiwemo jukumu la kutunga Sheria, Ibara ya 89 (1) ya Katiba, imetoa mamlaka kwa Bunge kutunga Kanuni za Kudumu kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kutekeleza shughuli zake.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad