Fahamu Hatua kwa Hatua Jinsi Rais wa Marekani Anavyopatikana

 


KUELEKEA uchaguzi wa kwanza wa urais Marekani, uliofanyika Desemba 1788 hadi Januari 1789, mtindo wa kumchagua na kupata rais, ulisababisha vichwa vya mababa waasisi wa taifa hilo viume.


Anachaguliwaje?


Ilikuwa mwaka 1787 baada ya Kongamano la Kikatiba lililofanyika Philadelphia, Marekani, katikati ya Septemba mwaka huo. Wazo la kwanza lilikuwa Rais achaguliwe na Bunge, kwa maana ya Congress. Yaani wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na maseneta wapige kura kumchagua rais.


Wazo hilo lilipingwa kwa kuonekana kungekuwa na kuingiliana kwa nguvu za mamlaka. Yaani mhimili wa uwakilishi (watunga sheria) kuwa na nguvu ya kumchagua mkuu wa utendaji, rais. Wazo la pili lilikuwa kuwapa fursa wajumbe wa mabaraza ya uwakilishi na seneti za majimbo ndio wachague rais.


Wazo hilo pia lilipingwa kwa kuonekana mamlaka ya serikali kuu yangekuwa yanategemea serikali za majimbo. Si kwamba haikufikiriwa kuhusu umma kumchagua rais kwa kura za moja kwa moja, yaani kura za umma (majority votes). Ilijadiliwa, lakini wajumbe wa kongomano la katiba walitilia shaka uwezo wa wananchi kuchagua rais bora.


Mmoja wa mababa waasisi wa Marekani, Alexander Hamilton, mwanasheria, vilevile mwanajeshi, ndiye akaibua hoja, kwamba kuwepo chombo chenye watu wenye uwezo wa kuchambua sifa za mtu anayepaswa kuwa rais. Hicho chombo ndicho kipewe mamlaka ya kuchagua.


Wazo hilo ndilo likawa sababu ya Katiba ya Marekani, Ibara ya pili, sehemu ya kwanza, kutoa maelekezo kuwa kila jimbo litachagua wajumbe idadi sawa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Seneti, ambao jumla yao wataunda chombo cha wachaguzi wa rais, yaani electors.


Hicho chombo ndicho huitwa electoral college. Na kura ambazo hupigwa na wajumbe wa chombo hicho, hufahamika kama kura za majimbo. Na kwa sasa, jumla ya wajumbe wa electoral college ni 538. Ili mtu achaguliwe kuwa rais anahitaji kupigiwa kura za majimbo angalau 270.


Idadi hiyo ya wajumbe wa electoral college imepatikana katika hesabu hii; Marekani kwa sasa ina wajumbe wa Baraza la Wawakilishi 435 na maseneta 100. Jumla 535. Mabadiliko ya 23 (XXIII) ya Katiba ya Marekani mwaka 1961, yaliipa hadhi Washington DC, wilaya kuu na makao makuu ya nchi kuchagua wajumbe wa electoral college. Wajumbe wa Washington DC ni watatu, hivyo kwa kujumlisha na 535, jumla ni 538.


Wajumbe 538 wanavyopatikana


Kwanza, wajumbe wa electoral college hawapaswi kuwa na kiapo cha utumishi mwingine wa umma, iwe serikalini au chombo chochote. Mjumbe wa chombo hicho cha kupiga kura hatakiwi kuwa na rekodi ya uhalifu, hasa uhaini, au kwa namna yoyote awe amewahi kushirikiana na nchi au jeshi la taifa lolote dhidi ya Marekani.


Mchakato wa kuwapata wajumbe wa electoral college huanza ndani ya vyama. Kipindi cha uteuzi wa wagombea urais kwenye vyama (primary election), vyama hufanya pia uchaguzi wa kuwapata wajumbe wa kwenda kuchaguliwa kuwa wapigakura wa majimbo.


Watu wanaopendekezwa na vyama kuchaguliwa kuwa wapigakura wa majimbo, huitwa slates. Wanachama wa vyama, wakati wakipiga kura za maoni kuchagua wagombea, vivyo hivyo huchagua majina ya slates.


Majimbo ya Oklahoma, Virginia na North Carolina, vyama huchagua majina ya slates kwenye makongamano ya kitaifa ya kupitisha majina ya wagombea urais. Hivyo wajumbe wa mikutano ya taifa ya vyama ndio huchagua slates, badala ya wanachama kuchagua moja kwa moja.


Jimbo la Pennsylvania, lenyewe lina utaratibu wake wa vyama kupendekeza slates wao. Wao hutaka kila mgombea, timu yake ya kampeni ipendekeze majina ya watu ambao wanawaamini wanafaa kuwa slates. Kisha mgombea aliyeshinda mchakato wa kura za maoni, majina yaliyopendekezwa na timu yake ya kampeni ndio yanapitishwa na chama.


 


Baada ya vyama kuwasilisha majina ya wanaowapendekeza kuwa wapigakura wa majimbo (slates), huchukuliwa na kuambatanishwa kwenye karatasi za wagombea urais. Hivyo, wananchi kwenye majimbo, siku ya uchaguzi hupiga kura kuwachagua wajumbe wa electoral college.


 


Kwa ufafanuzi, vyama huchagua slates, kisha wananchi wa majimbo hupiga kura kuchagua wajumbe wa chombo cha kupiga kura (electoral college) ambao huitwa electors. Hao electors ndio huamua nani awe rais wa Marekani.


 


Hivyo, Wamarekani kwa wingi wao huwa hawamchagui rais, bali huchagua wajumbe ambao hupiga kura kuchagua rais. Hata hivyo, mpango wa kutaka wananchi ndio wapige kura kuchagua wajumbe wa electoral college ni ili rais anayechaguliwa aakisi hisia za walio wengi.


 


Mgawanyo wa wajumbe


Wajumbe wa electoral college kwenye kila jimbo, hupatikana kwa uwiano sawa na idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, jumlisha maseneta wawili. Marekani, kila jimbo lina maseneta wawili, lakini wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hutegemea wingi wa watu kwenye jimbo hisika.


 


Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2010 Marekani, wastani wa watu 710,000 wanaongozwa na mwakilishi mmoja kwenye Baraza la Wawakilishi. Hivyo, kila eneo lenye watu 710,000, ama zaidi kidogo au chini kidogo, linastahili kupewa hadhi ya wilaya ya uchaguzi, hivyo kutoa mwakilishi.


 


Kwa utaratibu huo, majimbo yenye watu wengi yamekuwa na idadi kubwa ya wawakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi, wakati mengine yana mwakilishi mmoja. Hata hivyo, maseneta ni sawa katika majimbo yote. Kupitia mgawanyo huohuo, ni sawa na upatikanaji wa wajumbe wa electoral college.


 


Jimbo la California ambalo linaongoza kwa watu wengi, ndilo lina wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi. Jumla lina wawakilishi 53. Maseneta ni wawili. Jumla unapata 55. Idadi kama hiyo, 55, ndio sawa na wajumbe wa California kwenye electoral college.


 


California wajumbe 55, Texas 38, Florida na New York kila jimbo lina wajumbe 29. Illinois na Pennsylvania, wajumbe 20 kila jimbo. Ohio 18. Michigan na Georgia wajumbe 16 kwa kila jimbo. North Carolina 15. New Jersey 14. Virginia 13. Washington 12. Arizona, Indiana, Massachusetts na Tennessee wajumbe 11 kila moja.


 


Majimbo ya Maryland, Minnesota, Missouri na Wisconsin wajumbe 10 kila jimbo. Alabama, Colorado, South Carolina wajumbe tisa kwa jimbo. Kentucky na Louisiana wajumbe nane kila jimbo. Connecticut, Oklahoma na Oregon ni wajumbe saba kwa jimbo. Arkansas, Iowa, Kansas, Mississippi, Nevada na Utah wana wajumbe sita kwa jimbo.


 


Majimbo matatu ya Nebraska, New Mexico na West Virginia kila moja lina wajumbe watano. Hawaii, Idaho, Maine, New Hampshire na Rhode Island ni wanne. Majimbo ya Alaska, Delaware, Montana, North Dakota, South Dakota, Vermont na Wyoming, kisha wilaya ya Washington DC, kila moja ina wajumbe watatu. Jumla ndio unapata wajumbe 538 wa electoral college.


 


Kwa mujibu wa Katiba ya Marekani, Sehemu ya kwanza, kifungu cha nne, Bunge la Marekani (Congress), lilipewa mamlaka ya kuamua siku ya uchaguzi kikatiba. Yaani siku ya kuchagua wajumbe wa kura za majimbo na ile ambayo wajumbe hao watapiga kura kuchagua rais mpya.


 


Congress walishapitisha siku ya taifa ya uchaguzi. Ni Jumanne ya kwanza baada ya Jumatatu ya kwanza ya Novemba. Yaani, Jumatatu ya kwanza ya Novemba, siku inayofuata (Jumanne) ni siku ya taifa ya uchaguzi.


 


Ufafanuzi, endapo Novemba Mosi inakuwa Jumanne, hiyo haipaswi kuwa siku ya uchaguzi. Ni sharti Jumanne ya uchaguzi ifuate baada ya Jumatatu ya kwanza ya Novemba. Ikitokea Novemba Mosi ni Jumatatu, basi uchaguzi unakuwa siku inayofuata, yaani Jumanne ya Novemba 2.


 


Sasa, kikatiba kama ilivyopitishwa na Congress, kila Jumanne ya baada ya Jumatatu ya kwanza ya Novemba, kila baada ya miaka minne, wananchi hupiga kura kuchagua wajumbe wa kura za majimbo. Halafu, kila Jumatatu inayofuata baada ya Jumatano ya pili ya Desemba, wajumbe wa kura za majimbo hupiga kura kuchagua rais na makamu wa rais.


 


Wajumbe wa kura za majimbo wakishapiga kura kwenye majimbo yao, huzifunga kwenye bahasha maalum kisha kuelekezwa kwa Rais wa Seneti, ambaye ni Makamu wa Rais wa Marekani. Naye Makamu wa Rais haruhusiwi kufungua bahasha hizo za kura za majimbo, mpaka maseneta wawepo kushuhudia.


 


Makamu wa Rais (Rais wa Seneti), mbele ya maseneta, hufungua bahasha za kura za majimbo na kuhesabu. Baada ya hapo, Rais aliyeshinda hutangazwa rasmi. Na Januari 20, ndio siku ambayo rais huapishwa tayari kuanza majukumu mapya ya kiuongozi.


 


Biden na Trump


Kupitia muongozo wa kikatiba kuhusu siku ya taifa ya uchaguzi; Jumatatu ya kwanza ya Novemba mwaka huu ilikuwa Novemba 2, ndio maana uchaguzi ulifanyika Novemba 3. Siku hiyo ilikuwa maalum kwa Wamarekani kuchagua wajumbe wa kura za majimbo.


 


Mwaka huu, Jumatatu inayofuata baada ya Jumatano ya pili ya Desemba ni Desemba 14. Hiyo ndio siku ambayo wajumbe wa kura za majimbo, watapiga kura na kuzisaini, kabla ya kupelekwa kwa Rais wa Seneti ili zihesabiwe kwa uwazi na maseneta wote.


 


Huu ni mwaka wa uchaguzi wa Rais Marekani. Rais Donald Trump alitaka kushinda muhula wa pili kupitia chama cha Republican, wakati Joe Biden, Makamu wa Rais wa 47 wa Marekani, alicheza mpira mgumu aweze kuwa Rais wa 46 wa taifa hilo.


 


Utaratibu wa kupiga kura za mapema ulianza kupitia mitandaoni na kwa njia ya posta. Wamerekani kwa mamilioni walitumia haki yao ya kikatiba kuchagua rais wanayemtaka katika muhula ujao utakaonza Januari 20 mwakani.


 


Hata hivyo, siku yenyewe ya uchaguzi kwa Wamarekani wote wenye sifa ya kupiga kura ilikuwa juzi, Novemba 3. Hapo ndio walipigq kura za moja kwa moja kwenye vitu I vya kupigia kura. Kuchagua ama Trump na mgombea mwenza wake, Mike Pence waendelee au wawapishe Biden na Kamala Harris.


 


Sasa, Novemba 3, Wamarekani walivyokuwa wanachagua rais, ndivyo walikuwa wanapiga kura kuchagua wajumbe wa kura za majimbo. Wajumbe wa kura za majimbo picha zao hazipo kwenye karatasi za kupigia kura, bali jinsi walivyokuwa wanachagua mgombea wanayemtaka, ndivyo ilimaanisha kuchagua wajumbe wa kura za majimbo waliopendekezwa na chama chake.


 


Mathalan, mpigakura anampigia kura Trump. Hiyo kura yake itamaanisha kuchagua wajumbe wa kura za majimbo wa Republican. Chama kilichompa tiketi Trump. Inakuwa hivyo ili kuwezesha rais anayechaguliwa awe anaakisi matakwa ya walio wengi.


 


Rais anavyojulikana


Baada ya uchaguzi wa Novemba 3, Wamarekani wanaweza kupata uelekeo wa nani rais wao ajaye kulingana na kura. Anayepats wajumbe wengi zaidi wa kura za majimbo, anawasha taa ya kijani ya kuwa mshindi wa kiti cha urais.


 


Hivyo, bila shaka leo, Wamarekani watakuwa wameshamjua rais wa muhula utakaoanza Januari 20 mwakani. Ama ni miaka minne mingine kwa Trump au itaanza awamu mpya ya Biden ambaye kwa kiasi kikubwa ndiye ameshashinda.


 


Hata hivyo, hayo hayatakuwa matokeo rasmi. Mshindi rasmi wa uchaguzi wa Rais Marekani mwaka huu, atajulikana Desemba 14, baada ya wajumbe wa kura za majimbo kupiga kura rasmi na kusaini fomu zao, kisha hati zote zilizosainiwa kuhesabiwa na Seneti.


 


Kwa maana hiyo, yeyote atakayeshangilia matokeo baada ya uchaguzi wa Novemba 3 Marekani, ni wazi anasherehekea uelekeo wake wa kushinda, kwani mshindi rasmi ayakayetambulika na mamlaka za nchi hiyo, ni yule atakayethibitishwa na Seneti baada ya kuhesabu kura za majimbo.


 


Yupo mtu anaweza kujiuliza, inawezekana vipi watu washerehekee ushindi wakati matokeo ya mwisho yanakuwa bado? Jibu ni moja; wingi wa kura za wananchi kwenye jimbo husika, humaanisha wajumbe wa kura za majimbo wanakuwa wa mgombea aliyeongoza.


 


Kwa ufafanuzi; Trump ameongoza kwa kura za majimbo jimbo la Texas. Maana yake, wajumbe wote 38 wa electoral college watakaopiga kura za Texas Desemba 14 ni wa Republican, yaani ni kura za Trump. Na Biden hatakuwa na mpigakura kutoka Texas mwaka huu.


 


Biden ameshinda kwa wingi wa kura jimbo la California. Maana yake wajumbe wote 55 wa electoral college watakaopiga kura za California kumchagua rais Desemba 14, mwaka huu watakuwa wa kutokea Democratic. Ni kura za Biden.


 


Kwa mantiki hiyo, matokeo ya Novemba 3, yanatoa tafsiri ya mtaji wa kura za majimbo ambazo Trump na Biden wanakuwa nao. Nani atakuwa na wajumbe wengi kuliko mwenzake? Anayefikisha mtaji wa kura za majimbo 270, huyo ndiye anatarajiwa kushinda.


 


Siku ya uamuzi wa wajumbe wa kura za majimbo iliwekwa tofauti ili kuwezesha wajumbe hao kufanya uamuzi ambao utakuwa tofauti ikiwa wataona inafaa. Kwamba Trump anaweza kuwa na mtaji mkubwa wa wapiga kura ambao amewapa Novemba 3, lakini Desemba 14, mambo yakabadilika.


 


Inawezekana kabisa kupata wajumbe wengi wa kura majimbo lakini wasimpigie kura mgombea ambaye walipitishwa na chama chao wakampigie. Ndio maana kuna kitu huitwa “faithless electors” – “Wachaguaji wasio waaminifu.”


 


Wajumbe wa kura za majimbo ambao hupiga kura tofauti na matarajio, huitwa wachaguaji wasio waaminifu. Kwamba ni wachaguaji waliopitishwa na Democratic, kwa hiyo wangetarajiwa wamchague Biden, lakini wanamchagua Trump au mgombea kutoka miongoni mwa vyama vidogo.


 


Bahati nzuri, haijawahi kutokea mgombea aliyepata mtaji wa wajumbe wengi wa kura za majimbo, ashindwe kwenye majumuisho ya kura za Desemba kwenye Seneti. Hata hivyo, wasio waaminifu huwa hawakosekani.


 


Mwaka 2016, kulikuwa na kura saba za wachaguaji wasio waaminifu. Hesabu hiyo utaipata kupitia mgawanyo wa kura ulivyokuwa. Zingatia, wachaguaji (electors), ambao ndio hasa wajumbe wa kura za majimbo, hutokea kwenye vyama viwili, Democratic na Republican. Matarajio huwa katika mgawanyo wa kura 538 za majimbo, ama ziende kwa mgombea wa Republican au Democratic.


 


Mwaka 2016, wagombea wakuu walikuwa Donald Trump wa Republican na Hillary Clinton wa Democratic. Katika kura za majimbo, Trump alipata 304, Hillary 227. Jumla hapo ni 331. Wajumbe watatu walimpigia aliyekuwa Waziri wa Nchi wa Marekani, Collin Powell ambaye wala hakuwa mgombea. Kura moja alipigiwa mjamaa wa kidemokrasia, Bernie Sanders, ambaye pia hakugombea.


 


Mwanasiasa mkongwe Marekani, Ron Paul, naye alipata moja. Mwana-Republican ambaye ameshajaribu mara mbili kuwania tiketi ya chama hicho kuwa mgombea urais, John Kasich, alipigiwa kura moja, sawa na mwanaharakati Faith Spotted Eagle. Kimahesabu, kura hizo saba za Powell, Sanders, Ron, Kasich na Faith, zilitoka kwa wachaguaji wasio waaminifu.


 


Hiyo ikupe jawabu kuwa kupata wajumbe wengi wa kura za majimbo ni ushindi wa awali, lakini kibao kinaweza kugeuka. Katika Uchaguzi wa Rais Marekani, uliofanyika Novemba 8, 2016, Hillary alipata wajumbe 232, lakini alipigiwa kura 227 Desemba. Maana yake wajumbe watano hawakumpigia kura. Trump alipata wajumbe 306, lakini alipigiwa kura 304 Desemba, kwa hiyo wajumbe wawili hawakumchagua.


 


Athari yake ni kuwa endapo wajumbe wengi wa chama kimoja, watampigia mgombea wa chama pinzani, inaweza kutokea rekodi mpya kwa mgombea aliyezidiwa idadi ya wajumbe wa kura za majimbo kushinda urais Marekani. Na huo ndio msingi wa waasisi wa taifa hilo, kwamba kuwepo watu wenye uelewa mkubwa wa mambo ndio wachague rais. Na wawe na uwezo wa kupindua matokeo wanapoona kuna ulazima.


 


Hivyo, leo akishajulikana mshindi (bila shaka ni Biden), kisha tusubiri Desemba 14 kibao kitasemaje. Endapo hakutakuwa na mwenye kupata kura 270, basi Baraza la Wawakilishi ndilo litapiga kura kumchagua rais na Seneti watachagua Makamu wa Rais.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad