Miamba ya soka nchini Ufaransa Klabu ya Paris St-Germain ipo tayari kuonyesha jeuri ya fedha kwa kumsajili mchezaji ghali, bora na mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or, Cristiano Ronaldo endapo tu timu yake ya Juventus itaamua kumuuza msimu ujao.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 35 amejiunga na miamba hiyo ya soka ya Serie A akitokea Real Madrid mwaka 2018 huku kwa sasa akihakikishiwa kuingiza kibindoni paundi milioni 28 kwa mwaka kutoka kwa kibibi kizee hiko cha Turin
Mkurugenzi wa michezo kutoka PSG, Leonardo amesema kuwa kitu kisichotarajiwa kinaweza kutokea, hayo yanajiri baada ya kuulizwa swali kama upo uwezekano wa kunasa saini ya Ronaldo.
”Katika soka la sasa hufahamu nini kitatokea. Pengine kesho Cristiano Ronaldo anaweza kuamka na kusema anahitaji kwenda kucheza sehemu nyingine,” amekiambia chombo cha habari SGTV.
”Ni nani anayeweza kumnunua ? ni fumbo lililojifunga, PSG tukiwa ndani ya fumbo hilo. Yote kwa yote ni kuhusiana na fursa na kutegemeana na hali. Lazima tujiandae kwaajili ya dirisha la usajili na hicho ndicho tunachofanya. Tunavyo vipaumbele vyetu, orodha yetu lakini kitu kisichotarajiwa kinaweza kutokea.”
Licha ya janga la Corona kuyumbisha uchumi wa klabu nyingi barani Ulaya lakini kwa upande wake, Leonardo amejinasibu kuwa wapo vizuri.
Kwa upande mwingine PSG imeanza mazungumzo ya kumpatia kandarasi mpya mshambuliaji wa Brazil Neymar, huku nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 akifurahia kutia saini kandarasi hiyo ya miaka mitano.