Harmonize na Sarah Waagana Rasmi



NI rasmi sasa kwamba, zile tetesi kuwa ndoa ya staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na mkewe Sarah Michelotti inapumulia mashine, zina ukweli kwani wawili hao wameagana rasmi. Uvumi wa Harmonize au Harmo ulipata mashiko wiki iliyopita ambapo Sarah hakuonekana kwenye pati ya uzinduzi wa projekti mpya ya jamaa huyo ya Ushamba iliyofanyika makao makuu ya Lebo ya Konde Gang Music Worldwide yaliyopo Mbezi-Beach jijini Dar.

Lakini kama hiyo haitoshi, watu wa karibu na wawili hao wamekwenda mbele zaidi na kuvujisha majibizano ya wawili hao walipokuwa wakiagana baada ya penzi lao kusemekana kufi kia ukingoni. Kwa mujibu wa mawasiliano ya wawili hao, Novemba Mosi ilikuwa ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa (birthday) ya Sarah, lakini Harmo haikumshtua na wala hakukuwa na pati yoyote.

Zaidi, mawasiliano ya wawili hao yanaonesha wakiagana ambapo Harmo anamshukuru Sarah kwa kuwa naye yapata miaka mine hiyo kumtakia kila la heri kwenye maisha yake. Kwa upande wake Sarah, naye anamjibu Harmo kwa kumtakia maisha mema.

Taarifa za ndani zinaeleza kwamba, hali ya uhusiano wao haijawahi kutengamaa tangu kipindi kile cha skendo ya Sarah kudai kumfumania Harmo na yule video queen aitwaye Nicole Mbaga aliyeuza sura kwenye Video ya Bedroom ya Harmo. Habari za ndani zinadai Sarah ameshatimkia nchini kwao Italia.

Katika utetezi wa msanii wake, meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ alipoulizwa kuhusu ndoa ya msanii wake kuvunjika alisema; “Kwanza watu wanatakiwa watambue kitu kimoja kwamba yale ni maisha yao binafsi.”

Wakati Meneja wa Harmo akifafanua hayo, Sarah kwenye ukurasa wake wa Instagram amekuwa akirusha tu mafumbo; “Kulipiza visasi siyo jambo ninalolipendelea, utabaki na ujinga wako mwenyewe, habari za asubuhi.”

Harmo na Sarah wanadaiwa kufunga ndoa ya siri Septemba 7, mwaka jana jijini Dar es Salaam na kufanya sherehe iliyohudhuriwa na watu wachache jambo ambalo liliwafanya wengi kuingiwa na hisia hasi kuwa huenda wawili hao walikuwa wanatafuta kiki.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad