Huku marais na viongozi duniani tofauti wakiendelea kummiminia pongezi rais mteule wa Marekani Joe Biden baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu nchini humo - baadhi ya viongozi tajika wameonekana kukaa kimya.
Salamu nyingi za kumpongeza zilifuatiwa na taarifa kwa umma zikizungumzia kuhusu uhusiano mzuri na ushirikiano wa Marekani na umuhimu wa kufanya kazi na taifa hilo kuhusu masuala nyeti duniani. Viongozi hao walitoka Uingereza , wengi kutoka mataifa ya Ulaya , barani Asia, mashariki ya kati Afrika na Amerika.
Wapinzani wakuu China na Urusi
Serikali za Urusi na China zimenyamaza kwa siku kadhaa kabla ya kutoa taarifa kuhusu suala hilo, hatahivyo Jumatatu hii walizungumzia kuhusu jinsi walivyopokea matokeo hayo ya uchaguzi wa Marekani.
Urusi ilisema kwamba itasubiri matokeo yote rasmi kutangazwa na pingamizi zozote za kisheria kuamuliwa.
Ijapokuwa rais Vladmir Piutin alimpongeza Donald Trump 2016 wakati huu hajampongeza rais mteule Joe Biden.
Putin mara kwa mara amekuwa akisema kwamba yuko tayari kufanya kazi na kiongozi yeyote wa Marekani ili kuimarisha uhusiano mzuri kati ya mataifa hayo mawili.
China pia ilizungumzia kuhusu vikwazo vya kisheria ambavyo vimeangaziwa katika matokeo hayo huku rais Xi Jinping akijizuia kumpongeza Biden.
Uhusiano kati ya Washington na Beijing hauko katika hali nzuri baada ya miongo kadhaa , kutokana na mzururu wa vikwazo vilivyowekwa na utawala wa rais Donald Trump na pingamizi yake kuhusu uwanja wa teknolojia, msako wa viongozi Hong Kong na mlipuko wa virusi vya corona.
Lakini Biden amekuwa mkoasoaji mkubwa wa China na Jinping, akiahidi kuendeleza shinikizo na msimamo mkali dhidi ya Beijing.
Rais Erdogan wa Uturuki na aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani ambaye hivi sasa ndiye rais mteule wa taifa hilo Joe Biden
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ni kiongozi mwengine ulimwenguni ambaye bado hajatuma ujumbe wa pongezi kwa Joe Biden.
Licha ya kumkaribisha Joe Biden nchini mwake wakati alipokuwa makamu wa rais 2016, Erdogan ameendelea kunyamaza.
Hatahivyo wachambuzi nchini Uturuki wamezungumzia kuhusu mabadiliko yanayotarajiwa katika utawala wa Joe Biden., huku wanaounga mkono serikali ya Uturuki wakitofurahishwa na ushindi wa Biden.
Mojawapo ya vyanzo vya hofu kati ya Ankara na Washington ni majukumu ambayo Uturuki imejitwika nchini Syria.
Uhusiano mzuri kati ya Bin Salman na Trump
Ikumbukwe kwamba Saudia ambayo hadi kufikia siku ya Jumapili ilisalia kimya , hatimaye ilimpongeza rais huyo saa 24 baada ya matokeo hayo kutangazwa rasmi nchini Marekani.
Mwanamfalme Mohammed Bin Salman - kiongozi wa Saudia alimpongeza Biden na Kamala Harris na kuzungumzia kuhusu uhusiano wa karibu kati ya mataifa hayo mawili kulingana na chombo cha habari cha serikali SPA.
Trump alimlinda dhidi ya ukosoaji mkali wa kimataifa kuhusu ukiukaji wa haki za kibinadamu - mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi na uvamizi wa Yemen.
Masuala yote haya pamoja na uhusiano kati ya mataifa hayo mawili huenda yakaangaziwa upya na utawala mpya wa Joe Biden.