Wakati Yoweri Tibabuhurwa Kaguta Museveni alipochukua madaraka kuongoza Uganda mwaka 1986 alikuwa kijana wa miaka 42. Miaka 34 baadaye anaingia kwenye kinyang’anyiro cha kutetea kiti chake dhidi ya ‘mjukuu wake’ wake John Katumba, ambaye wakati anazaliwa rais huyo mkongwe kuliko wote Afrika mashariki alikuwa ametimiza miaka 28 madarakani.
Katumba ni mgombea binafsi wa nafasi ya urais, pamoja na Henry Tumukunde Kakurugu, na Nancy Linda Kalembe. Kura za maoni zimempendelea kijana huyo ambaye alipata asilimia 70 za ushindi, huku Museveni akipata asilimia 15, na Robert Kyagulanyi akiambulia asilimia 17. Umri wake umekuwa na gumzo ambapo duru za kisiasa zimebainisha kuwa ni ishara ya mafanikio ya demokrasia.
Inaelezwa kuwa kulingana na umri wake, harakati za siasa jinsi zilivyo zinamfanya kuwa miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa siku zijazo pamoja na kugombaniwa na vyama vya kisiasa.
Aidha, vijana katika ukanda wa Afrika mashariki wamepewa ujumbe kwa hatua ya John Katumba kuwa na ari, matumaini, uthubutu na dhamira halisi ya kuwatumikia wananchi na kutuma ujumbe kuwa kikwazo cha umri wa wagombea hakiwezi kuwa na manufaa tena na kwamba hizi ni zama za mabadiliko ya uongozi kwenda kwa kizazi kipya.
Katumba anawakilisha kizazi kilichosoma historia ya hekaheka za Museveni kushika madaraka zilizoanzia nchini Tanzania, ambako amewahi kushiriki mkutano maarufu unaojulikana kama Kongamano la Moshi ‘The Moshi Conference’ wa wapigania ukombozi wa nchi hiyo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania.
Aidha, duru za usalama nchini zinaeleza kuwa Museveni alinusurika kukamatwa na wanausalama wa uliokuwa utawala wa Iddi Amin katika kipindi ambacho alikuwa kiongozi wa kikundi cha Fronasa na baadaye NRM.
Wakati huo aliungana na wapigania ukombozi wengine kama vile ‘Kikosi Maalumu” cha Milton Obote, Tito Okello, Yusufu Lule (UNFL), David Oyite Ojok, Akena p’Ojok(SUM), William Omaria na Ateker Ejalu, Godfrey Binaisa, Andrew Kayiira na Olara Otunnu wa kikosi cha UFU.
Na sasa vijana wameamua kuweka wazi kuhitaji mamlaka ya kuendeleza mustakabali wao na kutuma ujumbe kwa kiongozi huyo mkongwe kuwa zama zake za kujivunia historia hii huenda zikafika tamati na si kigezo tena cha kusalia mamlakani.
Je kijana huyu ni nani anayepambana na majabali ya kisiasa?
Mgombea wa urais nchini Uganda John katumba
CHANZO CHA PICHA,JOHN KATUMBA/ INSTAGRAM
Jina lake ni John Katumba, alizaliwa mwaka 1996 katika kijiji cha Nsabwe kilichopo wilaya ya Mukoko, na sasa ana miaka 24. Taarifa zinabainisha kuwa historia yake inaanzia katika familia ya Kkonde ambapo wazazi wake walifariki dunia wakati akiwa na miaka miwili.
Makuzi yake yamekuwa mikononi mwa mlezi ambaye aliishi nae kitongoji cha Ntinda ndani ya jiji la Kampala. Familia yake inaishi huko Naalya-Kitatule jijini Kampala. Asili ya wazazi wake ni wilaya ya Buikwe iliyopo katikati ya nchi hiyo.
Elimu ya msingi alisoma katika shule ya Zion Hill huko Buikwe, kisha masomo ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha sita wilayani Mukono. Mlezi wake ndiye aliyekuwa akiwajibika huduma zote za elimu.
Baadaye alijishughulisha na uoshaji wa magari ili kupata fedha za kujikimu ambazo zilitoa mchango katika malipo ya karo za shule. Shahada ya kwanza ya usafirishaji aliipata katika Chuo Kikuu cha Makerere mapema Januari mwaka huu.
Novemba 3 mwaka huu Tume ya Uchaguzi ilipitisha jina lake baada ya kukidhi kigezo cha wadhamini 100 kutoka wilaya 98 nchini humo. Katumba akuwa mgombea kijana kuliko wengine 10 nchini humo akiwa anaungwa mkono na marafiki, wanafunzi wenzake wa zamani wa Chuo cha Makerere pamoja na kundi kubwa la vijana ambao wanamsapoti kwenye mbio za urais. Anagombea dhidi ya wanasiasa wenye uzoefu na hekaheka za uchaguzi nchini humo.
Matunda ya kubadili katiba
Taarifa za Tume za Uchaguzi zinabainisha kuwa hakuna kijana kama yeye ambaye amewahi kuwania urais katika historia ya Uganda. John Katumba ni zao la mabadiliko ya kikatiba ya mwaka 2018 ambayo yaliondoa kifungu cha 102b kilichoeleza kigezo cha umri wa kugombea urais. katiba ya Uganda kabla ya mwaka 2018 ilikuwa inaweka kigezo cha sifa za kugombea urais ni kuanzia miaka 35 hadi 75.
Ahadi zake akishinda urais Uganda
Mwanasiasa huyo ameahidi kujenga viwanja vya ndege vya kisasa huko Nile magharibi jijini Arua, kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri,kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali,kuboresha huduma za jamii, kuzalisha ajira kwa vijana,kusimamia uhuru wa kujieleza, kulinda usalama wa raia na mali zao.
Nchi jirani zinajifunza nini katika siasa za Uganda?
Nchini Tanzania raia wake wanaruhusiwa kugombea urais endapo wametimiza kigezo cha umri wa miaka 40. Pia wagombea binafsi hawaruhusiwi katika kila ngazi kuanzia serikali za mitaa, udiwani,ubunge hadi urais.
wakati wa uhai wake Mchungaji Christopher Mtikila aliwahi kushinda kesi dhidi ya serikali kuhusu ruhusa ya wagombea binafsi kushiriki siasa za Tanzania. Katiba ya Tanzania inataka wagombea wote wawe wanadhaminiwa na vyama vya siasa.
Uganda wanao wagombea binafsi John Katumba, Nancy Linda Kalembe, Henry Tumukunde. Siasa za Uganda zinatoa somo kwa majirani zao kuwa umri sio kigezo cha kuwanyima raia kugombea nafasi yoyote. Pia inawezekana haki ya raia wote kuwa huru kugombea nafasi bila kudhaminiwa na vyama.
“Urais wa nchi hauhitaji umri bali maono ya mtu husika na dunia. Kuna watu wengi nje ya siasa ambao wanaweza kuwa na maono mazuri zaidi juu ya nchi zao. Watu wasidhani kuwa rais ndiyo kwamba una akili kubwa kuliko raia wengine, bali unaongoza jopo la watu wenye uelewa mpana katika kufanya maamuzi sahihi kwa nchi.
Kuwaamini na kuruhusu vijana katika umri huo kwa Uganda ni moja ya hatua nzuri ya kuwajengea uwezo wakikua na kuamini wanaweza kubeba majukumu ya uongozi mkubwa nchini muda wowote baada ya mifumo inayofanya vijana waamini kuwa kuna nafasi siyo kwa ajili yao kisa tu umri kuwa mdogo,” anasema Richard Ngaya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine na mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora.
“Uganda wanaonekana kutumia falsafa ya zamani ya Tanzania kwa sababu viongozi vijana wengi waliibuliwa kuanzia Mwalimu Nyerere mwenyewe, Dk. Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba, Joseph Butiku, na Spika Pius Msekwa. Wote walipata nafasi kubwa za uongozi katika umri chini ya miaka 40 na wengine chini ya miaka 30.
Dk. Salim Ahmed Salim kuteuliwa kuwa balozi Misri akiwa na umri chini ya miaka 25. Lakini miaka hii tumezoea kuona nafasi za ubalozi ni za watu wanaokaribia kustaafu au wameshastaafu nafasi zao za utendaji serikalini, sina hakika na dira ya nchi juu ya mambo mbalimbali na namna inavyoamini kuwa hao wastaafu au wanaokaribia kustaafu wanaweza kufanikisha nchi ikafikia malengo,”
Je, anatuma ujumbe gani kwa vijana?
Katibu mkuu wa Umoja wa Wanawake Dodoma, Diana Madukwa ni miongoni mwa viongozi vijana walioibuliwa na umoja huo ambao ni taasisi ya chama tawala CCM ameguswa na harakati zinazofanywa na John Katumba.
“Urais unahitaji busara nyingi, hekima na kutulia huyu kama kijana mdogo bado sana kufikia kugombea hasa kwa nchi za Afrika wakiwemo majirani zetu Uganda ambazo nyingi zimetoka kwa wakoloni, na hawakuziacha nchi hizi na uchumi wa kujitegemea.
John Katumba angefaa zaidi kugombea nchi za ng’ambo ambako walishajitawala kwa miaka zaidi ya 200 kama Marekani ambako mifumo yote huhitaji kuanza kujenga sijui uwanja wa ndege, flyovers, madaraja, hospitali, shule kwa kuwa kila kitu kipo ni kusimamia tu.
Ameongeza, “Lakini, anatufunza kuthubutu ni haki ya kila binadamu japo inabidi tuangalie uwezo wa kuimudu nafasi unayoiomba.
Uganda wana katiba nzuri, inatoa fursa kwa vijana kama huyu, kwahiyo si suala la urais tu, bali kijana huyu anawaambia vijana wa Afrika mashariki wanaweza kuupata udiwani, uenyekiti wa mitaa, uongozi wa jumuiya, ubunge na nafasi zingine zenye uwezo nazo,”
Ni wagombea wangapi wanawania urais Uganda?
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Jaji Simon Byabakama mapema mwezi huu aliviarifu vyombo vya habari kuwa Januari 14, mwaka 2021 ndiyo siku ya kupiga kura kuchagua rais mpya. Nafasi ya rais inajumuisha wagombea 11 ambao wamekidhi vigezo, hivyo kuruhusiwa kufanya kampeni tangu Novemba 19 mwaka huu.
Wagaombea hao ni John Katumba, Robert Kyagulanyi Ssentamu, Meja Jenerali Mugisha Muntu, waziri wa zamani wa usalama Henry Tumukunde,Norbet Mao, Joseph Kabuleta Kiiza, Patrick Amuriat Oboi, Fred Mwesigye, Nancy Linda Kalembe, Willy Mayambala na Yoweri Museven kwa kuwataja wachache.