Ifahamu Historia ya Ikulu ya Chamwino na Nyerere




BILA shaka wengi hawajui historia ya Ikulu ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma ambayo sasa anaishi Rais Dk. John Magufuli. Historia ya Kijiji cha Chamwino ambacho ndipo Ikulu ilipojengwa, kiliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1971.

 

Maana halisi ya jina la kijiji hicho inatokana na neno la Kigogo, Mwino likiwa na maana ya chumvi ambapo inaelezwa kwamba hapo awali kulikuwa na bonde la chumvi lililokuwa likitumika kwa matumizi ya nyumbani.

 

Kijiji hicho kipo katika kata ya Buigiri, tarafa ya Chilonwa na Wilaya ya Chamwino, kilomita 40 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma.

 

Aidha, kwenye eneo la Chamwino Ikulu, kuna nyumba za kisasa za tembe ambazo zilijengwa kwa maelekezo ya Mwalimu Nyerere sambamba na nyumba za watumishi wa Ikulu, ikiwemo nyumba ya mwandishi wa habari wa Rais na Mwandishi wa Rais ambao nao waliishi humo wakati Mwalimu Nyerere akihamasisha uanzishaji wa vijiji vya ujamaa mwaka 1971.

 

Mwalimu Nyerere alifika kijijini hapo Julai 10, 1971 na kukaa kijijini kwa muda wa miezi mitatu hadi Oktoba 30,1971 akiwa anaishi kwenye hema.



Kijiji hicho kilianzishwaa kutokana na kambi la vijana wa chama kilicholeta uhuru cha TANU (Tanu Youth League) katika eneo lililokuwa linaitwa Ipala Lyanhembo (fuvu la tembo) na kambi hiyo iliongozwa na Mzee Robina Ligoha.

 

Mwalimu Nyerere alitembelea kambi hiyo Mei 5,1969 kuona shughuli za uzalishaji wa zao la zabibu, ukakamavu na utamaduni ambapo katika hotuba yake kambini hapo alitoa agizo kwamba Watanzania wasiishi kama panzi, bali waishi kama nzige vijijini.

 

Tarehe hiyohiyo, yaani Mei 5,1969 hayati Mwalimu Nyerere alipanda Mlima Matingha ambao siku hizi unajulikana kwa jina la Muongozo palipojengwa Ikulu ya sasa ya Chamwino pia kuna nyumba ndogo mlimani ilijengwa kwa kumbukumbu yake kwa kupanda mlima huo wenye mawe makubwa ambayo hata Rais John magufuli hivi karibuni alipanda juu ya mawe hayo.

 

Alipopanda mlima huo alipendezwa na mandhari aliyoiona. Aliangalia mteremko wa mlima pande zote, alishauri kambi la vijana wa Tanu Youth League kuhama kutoka kitongoji cha Ipala Lya Nhembo kuja kitongoji cha Makungulu Chamwino ambapo kwa sasa ni kijiji cha Chamwino Ikulu.

 

Vijana wa kambi hiyo waliitikia wito hivyo mwaka 1970 kambi hiyo ilihamia mahali alipoainisha Baba wa Taifa na kusema hapo panafaa zaidi.

 

Pia nyumba zisizopungua 10 nazo zilijengwa mara baada ya agizo hilo. Aidha, Julai 10, 1971 ndipo Baba wa Taifa alifika rasmi kuzindua kijiji hicho na kisha akakaa kwa muda wa miezi mitatu akiiishi kwenye hema na kuhakikisha wananchi wanaanza kuhamia kijijini hapo.

 

Kadhalika Julai 11, 1971 alianza shughuli za kufyatua matofali ya nyumba za wazee na wasiojiweza kwa balozi wa kwanza wa kijiji hicho, Leng’aisi Mayai. Mzunguko wa shughuli alizofanya Baba wa Taifa kijijini hapo kuwa ni pamoja na kupangiwa mabalozi mbalimbali katika kijiji kufyatua matofali na kujenga nyumba. Mwalimu Nyerere pia alishiriki kuchimba mitaro kwa ajili ya usambazaji wa maji kijijini hapo.



Shughuli nyingine zilizofanyika ni kusimamia makatapila kufyeka miti maeneo ya mashamba, mbuga ya Madima ambapo waligawiwa wananchi kulima eneo hilo na pia kijijini hapo kuna mbuyu uitwao Mwalimu J.K Nyerere kwa kumbukumbu kwani alikuwa anafanyia mikutano na wanakijiji hapo.

 

Aidha, Mwalimu alishiriki kufyatua matofali kwa kutumia mashine iliyokuwa inatoa matofali 12 kwa wakati mmoja. Matofali hayo ndio yaliyotumika kujengea Ikulu ndogo iliyojengwa mwaka 1971 lakini hivi sasa nyumba hiyo inatumika kama nyumba ya wasaidizi wa Rais na huduma mbalimbali za kijamii.

 

Matofali hayo pia yalijenga ukumbi wa kijiji wenye ofisi za watendaji wa kijiji, zahanati, shamba la mifugo ya ng’ombe wa kisasa wa maziwa na mbuzi wa kisasa, kuku wa kisasa, nguruwe, josho la mifugo na nyumba za watumishi wa serikali ya kijiji.

 

Mwalimu pia alishiriki katika kujenga nyumba za matofali ya kuchoma kwa wanakijiji ambao alishirikiana nao kucheza bao hasa na wazee kwenye mti wa Mnyinga uliopo kitongoji cha Kambarage baada ya saa za kazi, mti huo upo hata sasa.

 

Kijiji hicho cha Chamwino ikulu kilianza na vitongoji sita vya Kambarage, Mwongozo, Umoja, Maendeleo, Azimio na Ukombozi. Majina hayo yote yalibuniwa na Mwalimu Nyerere.

 

Kadhalika, kuna nyumba zaidi ya 40 zilizojengwa mwaka 1974 baada ya Mwalimu kuhamasisha wananchi kuwa na makazi bora ambapo wananchi walifyatua matofali huku wakikopeshwa vifaa vya ujenzi na Benki ya Nyumba (THB).



Mwalimu Nyerere alipeleka ng’ombe wa maziwa 20 kijijini hapo, akatengeneza ranchi yenye ukubwa wa ekari 640 ambayo ilizungushiwa uzio. Ranchi hiyo ipo eneo la Tairama. Baba wa Taifa alianzisha mradi wa msitu wa kupandwa Chamwino Ikulu mwaka 1982.

 

Msitu huo ulipandwa na Serikali chini ya usimamizi wa Wilaya ya Dodoma vijijini na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Sweden (SIDA).

 

Eneo la msitu lina zaidi ya hekta 100 likizunguka kijiji pamoja na miti iliyopandwa pande zote mbili za barabara kutoka Chamwino Ikulu hadi Buigiri na kufanya eneo hilo kuwa na ukanda wa kijani.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad