Jamaa Wamdai Bosi Wao Milioni 350, Wamwangukia JPM



JAMAA zaidi ya 20 ambao ni wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya Elerai Construction Company LTD ya jijini Arusha, inayomilikiwa na tajiri Samwel Lema wamesema wanamdai bosi huyo stahiki za mishahara yao kiasi cha shilingi milioni 350.


 


Wafanyakazi hao wamemuomba Rais Dk John Pombe Magufuli awasaidie kupata stahiki zao hizo ambazo hawajazipata tangu walipoachshwa kazi mwezi Machi, mwaka huu.


 


Wafanyakazo hao wameyasema hayo jana walipokuwa wakizungumza na vyombo vya habari jijini Arusha na kueleza malalamiko yao ya kutokulipwa stahiki zao ikiwemo mishahara na hivyo kuwasababisha kuishi kwenye mazingira magumu.


 


Wafanyakazi hao wamesema mkurugenzi wa kampuni hiyo, Lema amewaachisha kazi na hataki kuwalipa stahiki zao kiasi cha shilingi milioni 350 baada ya kufanya Kazi kwa miaka 20.


 


Akiongea kwa niaba ya wenzake kiongozi wa wafanyakazi hao ,Samweli William amedai kuwa walipokea barua za kuachishwa Kazi tangu mwezi Machi mwaka huu kwa madai kwamba Kampuni imeshindwa kujiendesha kutokana na ukata uliosababishwa na tenda za Ujenzi kupungua.


 


Amedai kuwa barua hizo zilielekeza kuwa watalipwa stahiki zao ikiwemo mishahara na kiinua mgongo,lakini hadi kufikia mwezi huu Mkurugenzi huyo ameshindwa kuonyesha nia ya kuwalipa licha ya kumkumbusha Mara kadhaa ,badala yake amekuwa akiwajibu kwa jeuri kwamba hana fedha.


 


Pia wamemtuhumu Mkurugenzi huyo kushindwa kupeleka michango yao katika mifuko ya hifadhi ya kijamii licha ya kukatwa mishahara yao kila mwezi,jambo ambalo ni kinyume cha sheria na wamemwomba Rais Magufuli kuwachukulia hatua waajiri wa namna hiyo wanaoshindwa kuzingatia sheria za Kazi.


 


“Baada ya kuachishwa Kazi tumekuwa tukifuatilia stahiki zetu lakini amekuwa akitujibu kwamba hana fedha kwa sasa na tukitaka tukalalamike popote “ alisema Samweli.


 


Akiongelea tuhuma hizo ofisini kwake,Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Elerai Construction ,Samweli Lema alikiri kuwaachisha kazi Wafanyakazi hao ,akidai kwamba Wafanyakazi hao wamechangia Kampuni yake kuyumba kimapato kutokana na hujuma za kimapato walizozifanya.


 


Lema ambaye pia ni mmiliki wa hotel ya kitalii ya Joshman na Kampuni ya Northern Engineering LTD zote za jijini hapa, alisema Wafanyakazi hao wameisababishia hasara Kampuni yake kupitia miradi mbalimbali ya Ujenzi waliokuwa wakisimamia.


 


“Niliishi na Wafanyakazi hao kama ndugu zangu na niliwaamini kupita kiasi ,lakini sikujua kumbe walikuwa wakisababisha hasara ,nimekuja kugundua tayari Kampuni imeyumba kila Mfanyakazi ameshavuna Mali za kutosha na wengine wanamagari zaidi ya matatu ya kifahari , Nyumba za maana na Maduka” alisema Lema.


 


Alisema hujuma hizo zilichangiwa na meneja wake aliyemtaja kwa jina la John Tarimo ambaye alikuwa akishirikiana na Wafanyakazi hao kuhujumu kampuni hiyo kupitia miradi mbalimbali ya Ujenzi.


 


“Nilifikiria kuwafungulia mashtaka Mahakamani na nilishaandaa mawakili wangu watatu lakini nimefika mahali nikaona haina haja cha msingi nimeamua kumwachia Mungu” alisema Lema.


 


Alisema kwa sasa Kampuni yake haina miradi mingi ya Ujenzi na anachokifanya kwa sasa ni kumalizia miradi iliyopo ili aweze kuachana shughuli za Ujenzi na anatafakari kufanya kazi nyingine.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad