BAADA ya kubaini kuwa huenda Simba ikawakosa washambuliaji wake wawili tishio Chris Mugalu na Meddie Kagere kutokana na majeraha, kocha wa timu hiyo Sven Vandenbroeck, ameweka mikakati ya kumtumia mshambuliaji wake mkongwe, John Bocco kuwamaliza Yanga.
Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Novemba 7 katika Uwanja wa Mkapa ambapo taarifa kutoka Simba zinaeleza kuwa huenda timu hiyo ikawakosa washambuliaji wake wawili, Kagere na Mugalu ambao ni majeruhi.
Simba mpaka sasa kwenye eneo la ushambuliaji, ina wachezaji John Bocco na Charles Ilanfya ambao ndio wazima ambapo Charles Ilanfya ameshindwa kupata nafasi ya kuanza kwani ndiye mshambuliaji aliyecheza mchezo mmoja tu wa ligi kuu huku Mugalu na Kagere wakiwa majeruhi.
Bocco katika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Mwadui FC alifanikiwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-0 lakini baadaye alitolewa kwa kilichodaiwa kuwa kocha Sven alikuwa akimlinda ili asipate majeraha yatayomfanya aikose mechi dhidi ya Yanga.
Vandenbroeck amesema kuwa licha ya Simba kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo wa kufunga, lakini timu hiyo inahitaji washambuliaji halisi kama Bocco.
“Simba ina wachezaji wengi sana wenye uwezo wa kufunga mabao lakini huwezi kuwa na uhakika wa matokeo bila ya uwepo wa washambuliaji halisia, tunawahitaji washambuliaji wote wawe fiti ili tuwe na uhakika wa kuchagua mshambuliaji wa kuanza kulingana na mchezo husika.
“Kulingana na washambuliaji wetu wawili kuwa majeruhi, hii inanipa wasiwasi wa kumtumia Bocco kwa muda mrefu kwani anaweza akaumia na ukiangalia tuna michezo migumu mbele yetu ikiwemo dhidi ya Kagera na Yanga na ndio maana kwenye mchezo uliopita nilimtoa mapema, nilihofia asiumie,” alisema kocha huyo.
Simba kabla ya kuwavaa Yanga Novemba 7 itakuwa na kibarua cha kuwakabili Kagera Sugar leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar.