RAIS Dkt. John Magufuli amesema kuwa hadhani kama chama chake kitapitisha mgombea wa urais anayezidi umri wa miaka 60 katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwani wapo vijana wengi wenye sifa za kuongoza, hivyo watapewa nafasi badala ya wazee ambao wamekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu.
Magufuli amesema hayo leo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, leo Jumatatu, Novemba 16, 2020, wakati akimuapisha Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, huku akisema kuwa, uongozi hauandaliwi bali ni Mungu ndiye anapanga nani awe kiongozi katika wadhifa upi na kwa wakati upi.
“Fanyeni kazi msiutafute Uongozi, vitu hivi vinapangwa, Mwinyi hakuutafuta Urais, Mimi sikujua kama nitakuwa Rais, sikuwahi kuomba hata Ujumbe NEC, Wajumbe walikuwa akina Lukuvi ila hakuupata Urais na sina uhakika kama ataupata Urais ana miaka zaidi ya 60.
“Lazima tuseme ukweli, Lukuvi ana miaka zaidi ya 60 ndio tukampendekeze awe Rais kweli? Maneno mengine yanaumiza ila lazima niwaambie mjiandae kisaikolojia na msipoteze hela zenu, hata wewe Kabudi huwezi kuwa Rais wa Tanzania wakati kuna Vijana kibao.
“Najua mmenyamaza (baada ya kuwaambia Wazee hamuwezi kuwa Marais), inawezekana umekaa na Jirani yako hapo ambaye atakuwa Rais ambaye ni Kijana zaidi, hii imemsaidia hata Hussein Mwinyi kushinda, Wapiga kura ni Vijana huwezi kuwapelekea Mzee sio saizi yao,” amesema Magufuli.