Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amewataka viongozi wa taasisi, wakala, bodi na vyuo vya mafunzo ya kilimo chini ya wizara kutowazuia watumishi wanapotaka kumuona na kuwasilisha shida zao za kikazi.
Amesema watumishi wa wizara hiyo kote nchini wana haki sawa na wale walio makao makuu kuwasilisha shida kwenda zao za kiutendaji ili azifahamu na kuzitatua badala ya baadhi ya wakuu wa taasisi kuwanyima ruhusa kwenda Dodoma kukutana na Katibu Mkuu.
Agizo hilo amelitoa jana (13.11.2020) alipotembelea na kuongea na watumishi wa Chuo cha Mfunzo ya Kilimo Kilombero (MATI) Katrin na wale wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ifakara vilivyopo Ifakara wilaya ya Kilombero.
“Mtumishi ana shida ya kuja kuniona (Katibu Mkuu) asizuiliwe na Mkuu wa Chuo au Mkurugenzi Mkuu bali aruhusiwe . Mimi ni kiongozi wenu njooni Dodoma wala hamhitaji miadi (appointment) kwa kuwa watumishi ndio nguzo ya mafanikio ya utendaji kazi wa wizara “alisema Kusaya.
Kusaya alisema kuwa katika zaiara zake kwenye taasisi,bodi na wakala wa chini ya wizara hiyo amebaini uwepo wa malalamiko ya watumishi kuhusu baadhi ya wakuu wa taasisi hizo kuwazuia watumishi kuwasilisha changamoto na matatizo yao kwa Katibu Mkuu hali inayowafanya wajisie unyonge na kupunguza morali wa ufanyaji kazi.
Kusaya aliwaeleza na kuwasihi wakufunzi na watumishi wasio wakufunzi kutambua wao ni sehemu ya wizara ya kilimo na wanastahili haki zote ikiwemo posho za masaa ya ziada (extra duty), mikopo toka Hazina yenye riba nafuu,fursa za kujiendeleza kimasomo na kupatiwa vitendea kazi ikiwemo magai,pikipiki na vifaa vya ofisi ili watekeleze kazi zao kwa ufanisi.
Akiwa katika Chuo cha MATI Ifakara (Katrin) Kusaya amerejea tena agizo lake kwa vyuo vyote 14 vya mafunzo ya kilimo vya umma kuhakikisha vinabuni miradi ya kujitegemea kwa kutumia ardhi kubwa iliyopo .
“Nataka kuona utofauti kati ya vyuo vya mafunzo ya kilimo vya zamani na vya sasa, mtu akiingia chuo cha kilimo akute mazingira yakifanana na kilimo kwa uwepo wa mashamba darasa bora ya uzalishaji mazao na kufuga mifugo kisasa “ aliagiza Kusaya
Katibu Mkuu huyo jana amefanikiwa kukamilisha kutembelea vyuo vyote 14 vya kilimo vya umma nchini na kuwa amewataka wakuu wa taasisi hizo kuanzisha mashamba darasa ili wanafunzi wajifunze kwa vitendo hali itakayokuza stadi na weledi kuwafanya watakapohitimu wawe maafisa ugani bora.
Katika hatua nyingine Kusaya ametoa onyo kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Ifakara kuacha mara moja kitendo cha kuzuia chuo cha mafunzo ya kilimo Ifakara kutumia ardhi iliyopo kufundishia wanafunzi kwa kigezo cha kutokuwa na kibali.
Naye Mkurugenzi wa Mafunzo,Utafiti na Ugani Wizara ya Kilimo Dkt.Wilhem Mafuru alisema wanampongeza Katibu Mkuu Huyo kwa kuvijali na kuvihudumia vyuo vya mafunzo ya kilimo ambavyo sasa vimepata taswira mpya chini tangu aingine wizarani.
Dkt.Mafuru aliongeza kusema Katibu Mkuu Kusaya amefanikisha kuunganisha wizara na wadau wa sekta binafsi hali iliyopelekea kazi ya kuhuisha mitaala ya vyuo vya mafunzo ya kilimo (MATIs) kuwezeshwa.
“Tunafarijika na uwepo wako Katibu Mkuu ndani ya wizara kwani umetusaidia kuboresha na kufanya vyuo vya mafunzo ya kilimo (MATIs) sasa zinatambulika na umma kupitia kazi zako tangu uteuliwe na Rais” alisema Dkt.Mafuru.
Katibu Mkuu huyo wa Kilimo aliagiza kuwa mashamba ya kituo cha utafiti TARI Katrin Ifakara yatumike kwa usawa kufanya shughuli za utafiti wa kilimo ikiwemo kufundishia wanafunzi wa chuo cha MATI Katrin bila vikwazo kwani taasisi hizo zote ni wizara moja .
“Kazi ya MATI Katrin ni kufundisha wanafunzi na wakulima kanuni bora na teknolojia za uzalishaji mazao hivyo sitopenda kusikia tena suala la uongozi wa TARI Ifakara ukiwanyima ardhi MATI.Wekeni utaratibu mzuri kila taasisi iwe na maeneo yake ya kudumu kutekeleza kazi zake “aliagiza Kusaya .
Akitoa salamu kwa niaba ya watumishi wa chuo cha MATI Katrin Mkuu wa chuo hicho Shadrack Kihombo alimshukuru Katibu Mkuu Kilimo kwa kutembelea taasisi hiyo na kutoa maelekezo yenye kukifanya chuo hicho kuwa bora.
Aliongeza kusema wanampongeza Katibu Mkuu huyo kwa kukiwezesha chuo hicho fedha Shilingi milioni 138 za kulipa madeni ya wazabuni mwaka huu hali iliyokuwa kikwazo cha utendaji kazi hususan upatikanaji chakula cha wanafunzi.
“Wewe ni kiongozi wa kwanza wa juu wa wizara yetu kufika hapa MATI Katrin tangu kimeanzishwa mwaka 2017 hatujawahi kutembelewa na kiongozi mkuu kama wewe. Tunakushuruku sana kwa jitihada zako za kuja kuona mazingira yetu tunayofanyia kazi na ahadi zako za kukisaidia chuo kiwe bora” alisema Kihombo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Ismail Mlawa alisema anaiomba wizara ya kilimo kutafuta soko la uhakika la mpunga kwa kutumia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutokana na wilaya hiyo kuzalisha kwa wingi.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa wito kwa wizara ya kilimo kusaidia kupatikana kwa maafisa ugani ili kila kijiji kiwe na mtaalam wa kilimo atakayesaidia kuelimisha wakulima uzalishaji mazao kwa kuzingatia hali ya soko ili kuondoa kero za wakulima kuzalisha aina moja ya zao mfano mpunga tu.
“Tunaomba wizara ya kilimo tusaidiane kuhamasisha wakulima kuachana na kilimo cha mazoea kulima zao moja tu badala yake walime mazao kulngana na hali ya soko ikiwemo ufuta,mahindi ya njano, korosho na hata mkonge yanayostawi vizuri Kilombero” alisisitiza Mlawa.
Akijibu hoja hizo Katibu Mkuu Kusaya alisema Wizara yake tayari imeanzisha Mfumo uitwao Mobile Watafiti unaolenga kuwafikia wakulima vijijini na kuwaelemisha uzalishaji wa mazao kulingana na ikolojia na hali ya soko ili wawe na uhakika wa kipato
Kusaya aliongeza kuwa wizara itaendelea kutafuta masoko ya mazao na kwa sasa inahamasisha wakulima kuanzia msimu huu kulima mahindi ya njano kufutia uwepowa soko la mazao hayo nchini Misri
“Tumepata soko la mahindi ya njano tani 20,000 kwa mwezi toka Misri hivyo nawasihi maafisa ugani tuwahamasishe wakulima walime zao hili pamoja na mazao mengine ili waongeze wigo wa kipato” alisema Kusaya.
Wizara ya Kilimo ina vyuo 14 na vituo 4 vya mafunzo ya mafunzo ya kilimo ambapo hadi kufikia jana Katibu Mkuu Kusaya amekamilisha kuvitembelea vyote na kukutana na watumishi tangu alipoteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli mwezi Machi mwaka huu kuwa Mtendaji Mkuu wa wizara.
Vyuo vyote vya mafunzo ya kilimo tayari vimepatiwa vitalu nyumba,pikipiki, vifaa vya Tehama ikiwemo kompyuta na baadhi kukarabatiwa ili kuviboresha vitoe mafunzo bora ya yatakayowezesha wataalam wengi wa ugani kupatikana ikiwa ni lengo la Seriklai ya Awamu ya Tano kukifanya kilimo kichangie zaidi katika ukuaji wa uchumi.
Mwisho
Imeandaliwa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Kilimo
IFAKARA
14.11.2020