KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze, ametamba kuwa tayari ameshawajua wachezaji hatari wa Simba wa kuwazuia mara watakapokutana nao tena kwenye Ligi Kuu Bara na mashindano mengine.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi dhidi ya Simba uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya 1-1.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kaze alisema kuwa safu ya kiungo ya Simba iliyokuwa inachezwa na Mzambia, Clatous Chama, Lous Miquissone, Mzamiru Yassin na Jonas Mkude ndiyo hatari inayohitaji kuchungwa.
Kaze alisema kuwa kabla ya mchezo huo aliwatahadharisha viungo wake wakabaji na mabeki kutowapa nafasi ya kumiliki mipira viungo hao kutokana na uwezo wao mkubwa wa kupiga pasi za mwisho ambazo zingekuwa hatari golini kwao.
“Kucheza na timu iliyokaa pamoja kwa misimu mitatu ambayo yote wanachukua ubingwa wa ligi siyo kitu kidogo, vijana wangu wanastahili kupongezwa katika hilo.
“Wachezaji wa Simba wanajuana na wana viungo wazuri wenye uwezo wa kupiga pasi za mwisho ambazo kama usingekuwa umakini wa mabeki wangu na viungo wakabaji basi wangetufunga.
“Simba wazuri sana kwenye safu ya kiungo pekee ambayo kama ukiidhibiti vizuri kwa kutoipa nafasi ya kumiliki mpira muda mrefu, basi unawafunga. Kosa hilo tulilifanya katika kipindi cha pili mara baada ya kuumia Lamine viungo wangu walikuwa wakicheza sana chini kutokana na kujilinda sana,” alisema Kaze