Jumla ya watainiwa 646,148 wa kidato cha pili kesho Novemba 9, wanatarajiwa kuanza mtihani wa upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili huku kidato cha Nne wakianza mtihani wa taifa Novemba 23 hadi Desemba 11, mwaka huu.
Akitoa ratiba hiyo leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza Mitihani la Tanzania (NECT), Dk. Charles Msonde amesema mtihani wa upimaji wa darasa la nne unatarajiwa kufanyika kwenye shule 4,948 za Sekondari Tanzania Bara na kwamba maandalizi yote yamekamilika.
Amesema kati ya watainiwa hao, wavulana ni 301,831 sawa na asilimia 46.71 huku wasichana wakiwa 344,317 sawa na asilimia 53.29.
“Mitahini hii inanza kesho Novemba 9 hadi 20 mwaka huu, aidha, wapo watainiwa wenye mahitaji maalum 731 na kati yao 406 ni wenye uoni hafifu, 55 ni wasiona, watatu ni wenye ulemavu wa kusikia na 267 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.
“Mwaka 2019 idadi ya watainiwa waliosajiliwa walikuwa 609,502, hivyo kuna ongezeko la jumla ya watainiwa 36, 646 sawa na asilimia 5.7 kwa mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana,” amesema Dk. Msonde.
Amesema mtihani wa taifa wa kidato cha Nne na Maarifa(QT) utafanyika Novemba 23 hadi Desemba 11, mwaka huu katuka jumla ya shule za sekondari na vituo vya mitihani 6,727 Tanzania Bara na Zanzibar.
“Jumla ya watainiwa 490,103 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha Nne mwaka huu ambapo kati yao watainiwa wa shule ni 448,164 na watainiwa wa kujitegemea ni 41,939.
“Kati yao watainiwa wa shule ni 448,164 waliosajili, wavulana ni 213, 553 sawa na asilimia 47.7 na wasichana ni 234,611 sawa na asilimia 52.3.
“Aidha, wapo watainiwa wenye mahitaji maalum 893 na kati yao 425 ni wenye uoni hafifu , 60 ni wasioona, 186 wenye ulemavu wa kusikia na 222 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili,” alisema Dk. Msonde.