Wagombea urais kutoka vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema kuwa wanasitisha kampeni zao hadi pale mgombea mwenzao Robert Kyagulanyi maarufu Kama Bobi Wine atakapoachiwa huru.
Wagombea hao wamesema ni vigumu kwao kuendelea na kampeni huku mgombea mwingine akiwa anaendelea kunyanyaswa na polisi kwa madai yasiyo na msingi.
Bobi Wine alikamatwa jana Jumatano Mashariki mwa eneo la Luuka baada ya polisi kumshtumu kwa kosa la kusababisha mikusanyiko ya watu ikiwa ni uvunjaji wa miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliowekwa na Tume ya Uchaguzi.
Na punde tu baada ya wafuasi wake kupata taarifa, walianza kuandamana wakidai aachiliwe huru.
Hata hivyo polisi imethibitisha kuwa watu watatu waliuawa wakati wa makabiliano kati yao na wafuasi wa Bobi Wine.
Taarifa ya polisi haikusema watu hao wamefariki vipi ingawa video na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zinaonesha watu waliotapakaa damu huku wengine wakioneshwa kutoweza kufanya lolote yaani wamepigwa risasi na kufariki dunia.
Aidha, taarifa ya polisi inasema watu 34 walijeruhiwa katika maandamano hayo.
Mgombea mwingine, Patrick Amuriat Oboi, pia amekamatwa.
Mikutano ya kampeni ya Bobi Wine imekuwa ikizuiwa na polisi katika matukio kadhaa.
Uganda itafanya uchaguzi wa urais Januari na hadi kufikia sasa polisi imekuwa ikihakikisha miongozi ya kukabiliana na janga la corona inatekelezwa.