Kina Mazrui Washukuru Waliopaza Sauti

 


Dar/ Unguja. Naibu Katibu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui na mwanachama mwingine, Ayoub Khamis Bakar wamewashukuru wananchi waliopaza sauti wakiitaka polisi kuwaachia huru au kuwafikishwa mahakamani baada ya kushikiliwa kwa siku 21.


Mazrui aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya ushindi wa kampeni za mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad akiwa na wanachama wengine, walikamatwa na polisi Oktoba 28 wakidaiwa kukutwa na vifaa vya kuingilia mfumo wa uchaguzi.


Hata hivyo, juzi Polisi iliwaachia kwa dhamana Mazrui na Bakar aliyewahi kuwa Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuanzia mwaka 2010-2016.


Shukran hizo zilitolewa jana na Mwanasheria wa ACT-Wazalendo, Omar Said Shabaan kwa niaba yao alipozungumza na Mwananchi kwa simu muda mfupi baada ya kuwatembelea katika makazi yao.


 

“Wameniambia niwashukuru wananchi wote waliopaza sauti kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii wakati wakiwa mahabusu. Wamefarijika sana,” alisema Shabaan. Wakili huyo alisema kitendo cha Mazrui na Ayoub kuachiwa ni hatua kubwa akisema kwa nyakati tofauti viongozi wakuu na wanachama walikuwa mstari mbele wakizitaka mamlaka husika kuwaachia huru.


 

“Bado tunasisitiza sheria ifuate mkondo wake, si kuwakamata na kuwaweka mahabusu kwa muda mrefu, kama mtu ana makosa apelekekwe mahakamani, lakini tunaamini hawa hawana makosa ni mambo ya kisiasa tu,” alisema.


Kuhusu hali zao, Shabaan alisema hazijatengemaa, kwani wana maumivu na watahakikisha wanafanya uchunguzi wa afya zao. Mazrui na Bakar watatakiwa kurudi polisi pindi watakapohitajika.


Katika hatua nyingine, Shabaan alisema Mahakama Kuu ya Zanzibar imeondoa ombi la ACT-Wazalendo la kuitaka itoe amri ya kulitaka jeshi la polisi kumfikisha mahakamani au kumuachia huru Mazrui na Bakar.


Shaban alisema ombi hilo lilitakiwa kusikilizwa jana, lakini halikusikilizwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo wahusika kutofika mahakamani badala yake walituma wawakilishi.


“Kwa kuwa polisi wamewaachia kwa dhamana, ni wazi dai letu linakufa kisheria na hatutakuwa na sababu ya kuendelea nalo,” alisema.

Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Haina maana kuwa Ugaidi na Vikosi vya kina jitto kuwa nia zenu ovu hamtofikishwa kunako sheria mkondoni.

    Wamwaga Damu nyie.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad