Mwanasiasa wa upinzani anayependelea sera za Ulaya nchini Moldova Maia Sandu ameshinda uchaguzi wa rais wa duru ya pili uliofanyika jana kwa kupata asilimia 56 ya kura.
Hayo ni kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa na tume ya uchaguzi ya Moldova wakati asilimia 99 ya kura zikiwa zimekwishahesabiwa.
Mpinzani wake Igor Dodon aliye rais wa sasa wa Moldova na ambaye wakati wa utawala wake aliegemea kusaka uungaji mkono wa Urusi amepata asilimia 43 ya kura.
Sandu mwenye umri wa miaka 48 alikuwa waziri mkuu kwa miezi kadhaa wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa Dodon kabla ya kuondolewa madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani.
Mwanasiasa huyo mwanamke amepigia upatu ushirikiano wa karibu kati ya Moldova na Umoja wa Ulaya kama njia muhimu ya kumaliza mzozo wa kiuchumi unaoliandamana taifa hilo la uliokuwa muungano wa kisovieti.