MWANAMUZIKI mkongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Antoine Christophe Agbepa Mumba almaarufu Koffi Olomide au Mopao Mokozi, amemnyooshea mikono na kumvulia kofia staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kisha kutamka; ‘You are the king…’ akimaanisha (Diamond) ni mfalme.
Kwa upande wake, Diamond au Mondi naye alimjibu; ‘No, you are the king and I’m the son of king…’ akimaanisha hapana, yeye (Koffi) ndiye mfalme na yeye (Mondi) ni mtoto wa mfalme
Koffi alimvulia Mondi kofia yake aliyokuwa amevaa aina ya kapelo ya kaki alipotua nchini usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita, akimfuata msanii huyo kwa ajili ya kolabo inayotajwa kuwa ya hatari.
Koffi alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar na kupokelewa kwa heshima zote na Mondi mwenyewe
Baada ya mapokezi hayo, Koffi alizungumza mambo mbalimbali hasa akimsifia Mondi kwa kazi nzuri anazozifanya na kueleza mpaka jinsi alivyomkubali mitandaoni na kusema anamuombea kwa Mwenyezi Mungu ili afanye vizuri zaidi.
Alipoulizwa siku aliyoanza kumsikia Mondi, Koffi au Papaa Ngwasuma alisema kuwa, ameanza kumsikia na kumfuatilia tangu miaka kumi iliyopita na kwa sasa ndiye mfalme wa muziki kwa watu wa kizazi chake kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Baada ya Koffi kuzungumza hayo, Mondi naye alisema kuwa, ana furaha mno kutimiza ndoto yake ya japo kumkaribia Mopao aliyeanza
kujizolea sifa katika tasnia ya muziki kwa zaidi ya miaka 30 sasa akiwa na umri wa miaka 64.
“Siamini macho yangu kuwa na mkongwe kama huyu ambaye hata sikuwahi kuota kuwa siku moja nitakuwa naye hata kwa ukaribu kama huu,” alisema Mondi akionekana mwenye furaha mno.
Alipoulizwa sababu ya ujio huo, Mondi alisema mkongwe huyo ametinga Bongo kwa ajili ya kufanya naye kazi ya muziki ambapo kuna wimbo wa pamoja wanatarajia kuutoa wa kufungia mwaka.
“Amekuja kuna kazi ya muziki tunataka kuifanya ambapo tutatoa wimbo wa pamoja ambao utatoka hivi karibuni na naamini utabamba sana.
“Si unajua Simba (Mondi) nikiwa na mkongwe kama huyu (Koffi) unafikiri kitaharibika kitu kweli hapo?” Alihoji Mondi kwa kujiamini na kuongeza;
“Basi mashabiki wa burudani watusubirie tu kuona hicho kitu ambacho tunatarajia kukitoa hivi karibuni ambacho nadhani kitatisha sana.”
Mopao anakuwa ni mwanamuziki mwingine kutoka Kongo kufanya kazi na Mondi baada ya wanamuziki Fally Ipupa na Innoss’B.
GPL