Watu sita wakiwemo Madaktari wamefungwa gerezani nchini China kwa kutoa viungo vya mwili kinyume cha sheria kwa watu waliofariki kutokana na ajali, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti juu ya hukumu hiyo.
Kundi hilo lilikuwa limelaghai familia za waliofariki kuwa wanachangia rasmi viungo vya mwili katika mashirika husika.
Kati ya mwaka 2017 na 2018 walitoa maini na figo kutoka kwa watu 11 katika hospitali ya Anhui.
Watuhumiwa hao sita wakiwemo Madaktari wanaohusika na ulanguzi huo wa viungo vya binadamu walisomewa mashtaka yao Julai mwaka huu kwa kosa la “kuharibu miili ya wafu kimaksudi” na kuhukumiwa kifungo cha kati ya miezi 10 na 28 gerezani.
China inakabiliana na upungufu wa viungo vya mwili na imekuwa na wakati mgumu kukidhi mahitaji ya raia.