Magari ya Ginimbi Kugawiwa Watoto Yatima




NI maajabu! Ndivyo unavyoweza kutafsiri wosia aliodaiwa kuachwa na bilionea wa Zimbabwe, Genius Kadungure ‘Ginimbi’ ambaye amezikwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika makazi yake huko Domboshava nchini humo.

 

 

Katika wosia huo imeelezwa kuwa bilionea huyo ambaye pia ni shemeji wa mzazi mwenza wa msanii maarufu nchini, Nasib Abdul ‘Diamond’, Zarina Hassan, aliagiza kuwa akifariki magari yake yote yauzwe na fedha zitakazopatikana zigawiwe kwenye vituo vinavyolea watoto maskini wanaoishi katika mazingira magumu.

 

 

Pia bilionea huyo aliyekuwa anakadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya Sh bilioni 200, aliagiza nguo zake za thamani, na viatu vyote vichomwe moto. Kwa mujibu wa gazeti la The Herald la nchini humo, maagizo ya bilionea huyo, yamewaacha midomo wazi wananchi wa Zimbabwe, wafuasi wake pamoja na familia yake kwa ujumla.

 

Bilionea huyo ambaye alijipatia umaarufu katika mitandao ya kijamii kutokana na mtindo wake wa maisha ya kifahari pamoja na uraibu wa magari aliokuwa nao, alifariki duniani Novemba 8 mwaka huu katika ajali ya gari iliyosababisha vifo vya watu wanne akiwamo yeye.

 

 

WOSIA WAKE WAIACHA FAMILIA MDOMO WAZI

Aidha, kwa mujibu wa gazeti la Zim Morning Post, familia ya bilionea huyo aliyekuwa na umri wa miaka 36, ilipigwa butwaa baada ya baadhi ya taarifa za wosia alioacha kuhusu mgawanyo wa mali zake kuvujishwa na mwanasheria wake aliyefahamika kwa jina la Brighton Pabwe.

 

Licha ya mwanasheria huyo kutokuweka hadharani wosia huo kwa madai kuwa bado ni mapema, inaelezwa kuwa kabla ya kifo chake, bilionea huyo aliandika wosia wa mali zake na kufafanua namna zitavyotakiwa kugawanywa pindi atakapokuwa amefariki dunia.

 

“Ginimbi aliagiza magari yake yote ya kifahari yauzwe na fedha hizo zigawiwe kwa vituo vinavyolea watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

 

“Pili aliagiza nguo zake zote za gharama viatu na mavazi mengine yachomwe moto,” kilieleza chanzo kimoja kilichomnukuu mwanasheria huyo. Hata hivyo, Wakili Brighton Pabwe pamoja na Wakili Jonathan Samkange ambao wote walikuwa wanasheria wa Ginimbi, walifafanua zaidi kuwa itachukua muda mrefu kutoa hadharani wosia rasmi wa gwiji huyo aliyejizolea umaarufu katika ukanda huo wa nchi za kusini mwa Afrika.

 

“Kwa sababu huyu alikuwa tajiri mkubwa, na yapo mambo mengi ya kuweka sawa, hatuwezi kutoka hadharani na kuonesha wosia wake ilihali bado mambo hayajakaa sawa, kwa hiyo wafuasi wake wasubiri lakini hatuwezi kusema kuwa ni lini,” alisema Wakili Pabwe.



MJOMBA WAKE ANG’ANG’ANIA LAMBORGHINI

Wakati wanasheria hao wakianika hayo, mtu moja aliyedaiwa kuwa ni mjomba wake, alijitokeza na kujirekodi video huku akisisitiza kuwa, yeye ndiye mrithi wa gari la thamani aina ya Lamborghini Aventado.

 

Gari hilo ni moja ya magari lukuki ya kifahari yaliyoachwa na marehemu Ginimbi ambayo ukikusanya magari hayo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni 3.1 na yapo kwenye himaya yake. Katika video hiyo iliyosambaa mitandaoni, mwanaume huyo alisema gari hilo linamtosha hivyo hahitaji kingine pindi familia itakapokaa kugawanya mali hizo.

 

MAGARI YA GINIMBI

Kwa miaka mingi, Ginimbi amekuwa akimiliki magari ya gharama kubwa na hakuficha wakati wowote kuonesha kila gari alilonunua kupitia mitandao ya kijamii. Wiki moja kabla ya kifo chake, Ginimbi alikuwa amenunua gari jipya la Lamborghini Aventador ambalo alilielezea kama kitu kipya cha kuchezea (new toy).

 

Kulingana na gazeti la Times Live, miongoni mwa magari yake ambayo ameyaacha ni pamoja na:

Rolls-Royce Ghost (2016 model)

Rolls-Royce Ghost (2020 model)

Rolls-Royce Wraith (ambalo alikufa akiwa analiendesha)

Bentley Continental GT (2014 model)

Bentley Continental GT W12 (2020 model)

Bentley Bentayga Bentley Mulsanne Lamborghini Aventador S Coupe Ferrari 488 Spider Mercedes G Wagon Brabus (2016 model)

Mercedes G Wagon G63 (2020 model)

Range Rover Vogue Autobiography (2019 model)

Range Rover Sport SVR (2019 model)

Range Rover Sport Lumma (2017 model)

Range Rover Sport (2018 model)

Range Rover Velar (2018 model)

Mercedes-Benz S Class (2014 model)

Mercedes-Benz S Class (2019 model)

Hata hivyo, hakuna chanzo huru cha kuthibitisha taarifa zilizotolewa na gazeti la Times Live ingawa Ginimbi anatambuliwa kuwa alikuwa ni mtu aliyekuwa na uraibu wa kununua magari ya kifahari.

 

SAFARI YA UTAJIRI WAKE

Wakati mazishi yake yakiendelea kuwa gumzo, upande wa pili utajiri wake pia nao umezidi kuwaweka watu njia panda kutokana na magari ya kifahari na majumba aliyokuwa anayamiliki kijana huyo.

 

Ginimbi, safari yake kimaisha aliianza mwaka 2000 kwa kuanza kujishughulisha na uuzaji wa mitungi ya gesi ambayo alikuwa akiisambaza majumbani mwa watu. Wakati huo akiwa na umri wa miaka 17 anaidawa kuifanya biashara hiyo ambayo ilimpatia uzoefu mkubwa uliomkutanisha na rafiki yake aliyekuwa anafanya kazi katika ofisi za Shirika la Ndege la Angola.

 

Kwa mujibu wa taarifa zake, hapo ndipo siri ilipojificha kwani tangu alipokutana na rafiki yake huyo, inaelezwa mambo yalimnyookea Ginimbi ambaye alianzisha kampuni yake ya kusambaza gesi ijulikanayo kama Pioneer Gases.

 

Kampuni hiyo ambayo sasa ni kubwa katika ukanda huo ina matawi nchi za Zimbabwe, Botswana na Afrika Kusini. Ndani ya miaka miwili alipata magari mawili ikiwamo gari la thamani aina ya Mercedes Benz S class.

 

Ginimbi alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Piko Trading ambayo ilikuwa inamiliki makampuni ya Rivonia Gases, City Centre Freight, Pioneer Gases and Quick Gases ambazo zote ofisi zake zipo katika nchi za Zimbabwe, Afrika kusini na Botswana.

 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad