Vita, njaa, vifo, maradhi – ni vitu ambavyo wengi wamevisikia na kuvifahamu kuhusu Afrika. Lakini sasa ni wakati wa kubadili mtazamo huu. Afrika ni bara la kushangaza ambalo ni tofauti kabisa na mabara mengine saba. Afrika ina utajiri katika urithi wa utamaduni wa kipekee, utajiri wa rasilimali za asili pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii. Nakukaribisha ufuatilie makala hii ili uweze kufahamu mambo 15 ya kushangaza na kusisimua kuhusu Afrika.
1. Mlima Kilimanjaro unapatikana barani Afrika. Mlima huu una urefu wa takriban meta 5,895 kutoka usawa wa bahari. Mlima huu unapatikana kaskazini mwa Tanzania.
2. Zaidi la asilimia 25 ya lugha huzungumzwa Afrika. Inaaminika kuwa kuna takriban lugha 2000 zinazozungumzwa barani Afrika. Lugha zote hizi zinatambuliwa na umoja wa Afrika. Nigeria pekee ina lugha hai 500.
3. Afrika ni bara pekee linaloanzia ukanda wa kaskazini wa joto hadi ukanda wa kusini wa joto. Ni bara lenye joto zaidi duniani na la pili kwa ukame baada ya Australia.
4. Afrika ni bara lenye watu wa umri mdogo zaidi. Zaidi ya asilimia 50 ya watu Afrika wako chini ya umri wa miaka 20, ukilinganisha na kiwango cha wastani cha dunia ambacho ni 30. Hivyo Afrika ina kiwango kikubwa cha watoto tegemezi chini ya umri wa miaka 15.
5. Chuo cha zamani zaidi kipo Afrika. Ni chuo cha Karueein kilichopo Morocco, kilianzishwa mnamo mwaka 859 BK na bado kinafanya kazi.
6. Afrika ni bara la pili kwa ukubwa pia ni bara la pili kwa kuwa na watu wengi. Afrika ina ukubwa wa kilometa za mraba 30,244,049 pamoja na idadi ya watu inayozidi 1,216,130,000.
7. Mto Nile ni mto mrefu kuliko yote Afrika. Mto huu una urefu wa kilometa 6,650 (maili 4,132) na umekatiza kwenye nchi 11.
8. Kisiwa kikubwa zaidi Afrika ni Madagascar, kinapatikana bahari ya Hindi na kina ukubwa wa kilometa za mraba 587,713. Pia kisiwa hiki ni cha nne duniani kwa ukubwa na cha pili kwa nchi kubwa ambazo ni visiwa.
9. Maporomoko ya maji ya Victoria yaliyoko mpakani mwa Zambia na Zimbabwe, ni moja ya maajabu ya dunia. Mto zambezi ni chanzo kikubwa cha maji ya maporomoko hayo.
10. Ziwa viktoria ni ziwa kubwa zaidi Afrika na la tatu duniani kwa ukubwa (Kilometa za mraba 69,485). Ziwa hili lipo eneo la maziwa makuu likihusisha Tanzania, Kenya na Uganda.
11. Afrika ni makazi ya mnyama mrefu na mkubwa zaidi duniani. Wanyama hao ni twiga na tembo ambao wote wanapatikana Afrika.
12. Kiboko ni mnyama hatari zaidi Afrika, ameuwa watu wengi zaidi kuliko waliouawa na mamba pamoja na simba.
13. Witwatersrand ya Afrika Kusini imezalisha karibu nusu ya dhahabu yote iliyochimbwa Afrika.
14. Kuna watu wengi wanaozungumza Kifaransa Afrika kuliko wale walioko Ufaransa.
15. Afrika na Ulaya imetengwa na bahari kwa karibu zadi kwa kilometa 14.3 kati ya Hispania na Morocco. Inasemekana kuwa nchi hizi ziko kwenye mazungumzo ya kujenga daraja ili kuziunganisha na kurahisisha usafiri.
Kwa hakika kuna mambo mengi mazuri kuhusu Afrika, lakini hatuwezi kuyaweka yote. Tunaamini kuna mengi mazuri na ya muhimu ambayo ingekuwa vyema tukayaweka. Hapa ndipo nafasi yako inatokea, ikiwa una jambo jingine zuri ulilopenda tuliweke au una maoni, tafadhali tuandikie hapo chini. Pia usisahau kuwashirikisha wengine makala hii.