Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya raia 110 wameuawa katika shambulizi baya lililotokea mwishoni mwa juma kaskazini mashariki mwa Nigeria. Edward Kallon, mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya kiutu nchini Nigeria, amesema watu wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki waliwauwa raia kwenye mji wa Koshobe na maeneo mengine kulizunguka jimbo la Borno.
Kallon amesema watu wengine wamejeruhiwa vibaya na kuna taarifa kwamba wanawake kadhaa wametekwa nyara. Amesema hilo ni shambulizi baya kabisa dhidi ya raia wasio na hatia kushuhudiwa kwa mwaka huu.
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amelaani vikali mauaji hayo. Hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na mauaji hayo.
Lakini kundi la Boko Haram na wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu katika kanda ya Afrika Magharibi, ISWAP wamekuwa wakifanya mashambulizi kwenye eneo hilo katika miaka ya hivi karibuni.