Klabu ya Waandishi wa Habari ya Kilimanjaro (MECKI) imelitaka Jeshi la polisi kuchunguza kwa weledi sababu za kifo cha mwanahabari wa kituo cha redio cha Kili FM, Benedict Kuzwa ili kuondoa wingu zito lililogubika tukio hilo.
Hoja ya MECKI inatokana na taarifa zinazodai kuwa siku hiyo saa 10:00 alasiri, alichukuliwa na gari lenye vioo vyeusi na hakupatikana hadi mwili wake ulipookotwa siku hiyo saa 3:30 usiku
Katibu mkuu wa MECKI, Nakajumo James aliliambia gazeti hili jana kuwa kwa vile tayari kuna shaka, ni wajibu wa polisi kuchunguza mawasiliano yake ya simu na kuwatafuta watu wanaosemekana walimchukua
Tayari familia ya mwandishi imegoma kuchukua mwili wa ndugu yao kwa ajili ya maziko, wakitaka uchunguzi mpya ufanywe kuhusu sababu za kifo cha ndugu yao, badala ya taarifa ya awali inayodai kilitokana na ajali.
“Hizi doubt (shaka) za sasa hivi polisi ndio wanazitengeneza kwa sababu wao wana wataalamu wa uchunguzi, wa kuanzia mawasiliano yake ya mwisho na hata watu wa mwisho kuwa naye ni kina nani,” alisema Nakajumo.
‘‘Sasa wanapochukulia kirahisi tu kwamba ni ajali kama vile mtu mwingine wa mtaani angechukulia haiwezekani lazima waonyeshe nguvu ya kimamlaka waliyonayo. Ni nani hao waliomchukua kwenye gari?”alihoji.
“Hilo gari linalosemwa ni la aina gani, lilimpeleka wapi. Lakini jingine wanatakiwa walichunguze ni eneo mtu anapogongwa kwanza kunakuwa na kishindo na kungekuwa na alama kama dereva alijaribu kushika breki.
“Nadhani ni wakati mzuri kwa polisi kutumia wataalamu wao wachunguze mawasiliano yake ya simu. Nani waliwasiliana naye mara ya mwisho. Hilo gari lililomchukua ni la watu gani. Haya maswali yanahitaji majibu.”
Kauli ya MECKI inatokana pia na kauli ya mjomba wa marehemu, Bryson Enirisho aliyedai kuna mazingira huenda ndugu yao alipata mateso eneo jingine na kwenda kutupwa njia panda ya Himo.
Emmanuel Kawala, ambaye ni kaka mkubwa wa marehemu, alisema familia imeamua kutozika mwili wa ndugu yao kutokana na kutoridhishwa na majibu ya awali ya uchunguzi wa sababu za kifo.
Mwili wa marehemu Kuzwa ulifanyiwa uchunguzi jana Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako ndugu wa marehemu walikataa majibu yaliyotolewa na kuomba uchunguzi urudiwe.
Kawala alisema majibu ya awali yanaonyesha ndugu yao alifariki baada ya kuvuja damu kwa madai ya kugongwa na gari, sababu ambazo wao wanazikataa kwa hoja kuwa kuna kila dalili kuwa aliuawa.
Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizopatikana juzi zilieleza kuwa kutokana na msimamo huo wa ndugu, chombo hicho cha dola kimefungua jalada la uchunguzi na tayari ndugu wa marehemu wameandika maelezo yao.
Kauli ya RPC Kilimanjaro
Kamanda wa polisi wa mkoa, Emmanuel Lukula aliwaambia wanahabari Novemba 12 kuwa taarifa za kuuawa ni uvumi na kusisitiza kifo chake kimetokana na ajali ya gari.
Kamanda Lukula alisema ajali hiyo ilitokea Novemba 7 katika mji mdogo wa Himo na kwamba mwandishi huyo alipata ajali hiyo wakati akitoka katika majukumu yake ya uandishi wa habari.
“Wapo wanaosema aliuawa lakini kilichotokea ni kwamba huyu mwandishi aligongwa na gari na lilimburuza kidogo na kuchubuka. Tukio lilitokea usiku wa saa 3:30 Novemba 7,” alisema.
Hata hivyo, juzi kupitia ukurasa wa Facebook, Upendo Kuzwa, ambaye ni dada wa marehemu, alipinga taarifa ya polisi kuwa mdogo wake alipatikana usiku wa Oktoba 7, akisema siku hiyo mdogo wake hakuwa amekufa.
“Si kweli. Si kweli mdogo wangu hadi Jumapili (Novemba 8) alikuwepo,” ameandika Upendo.
Kuchambua siasa na jamii
Enzi za uhai wake, Kuzwa alikuwa akiendesha vipindi viwili vya Kili Breakfast na Kili Drive, ambavyo vinaelezwa vilijikita katika kuchambua masuala ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na michezo.
Katika vipindi hivyo, mwandishi huyo alikuwa alikuwa akiendesha mijadala kwa njia ya simu ambazo waskilizaji walikuwa wakipiga kuchangia hoja zao.