Shirikisho la mpira wa miguu barani afrika CAF limeruhusu mashabiki kuingia uwanjani kwenye mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu michuano ya mataifa afrika AFCON 2021 kati ya Tanzania na Tunisia
Taarifa iliyotolewa na idara ya habari na mawasiliano ya shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF inasema.
‘shirikisho la mpira wa miguu afrika CAF limeruhusu watazamaji kwenye mchezo wa kufuzu AFCON kati ya Tanzania na Tunisia utakaochezwa Novemba 17, 2020 kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es salaam”.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa idadi ya watazamaji watakaoingia uwanjani ni asilimia 50 ya uwezo wa uwanja, TFF pia imeweka wazi inawasiliana na Serikali ili kukidhi matakwa ya CAF katika mechi hiyo.
Taarifa hii inafuatia baada ya siku chache zilizopita CAF kutoa taarifa kuwa michezo ya raundi ya 3 na 4 ya kufuzu fainali za AFCON mwaka 2021 itachezwa pasipo na uwepo wa mashabiki uwanjani ikiwa ni katika hatua za kujikinga na ugonjwa wa covid-19.
Mchezo wa kwanza kati ya Tunisia na Tanzania unachezwa Novemba 13 nchini Tunisia na mchezo wa marejeano utachezwa Novemba 17 dar es salaam.
Tunisia ndio vinara wa kundi J wakiwa na alama 6, nafasi ya 2 wanashika Libya wenye alama 3 sawa na Tanzania wanaoshika nafasi ya 3 na Equatorial Guinea ndio wanaoburuza mkia wakiwa hawana alama hata moja.