Mwanamume mweusi aliyekufa baada ya kupigwa na walinzi wa duka kuu amezikwa Jumamosi kufuatia maandamano yaliyotokea kulaani mauaji hayo. Joao Alberto Silveira, baba wa watoto wanne, alizikwa akiwa amevaa fulana nyeupe ndani ya jeneza lenye bendera ya timu ya soka aliyoipenda katika mji wa Porto Alegre.
Mamia ya watu waliandamana kote nchini, wengi katika matawi ya duka kuu la Carrefour wakibeba mabango yalioandikwa "Maisha ya Watu Weusi ni Muhimu", sawa na maandamano yaliofanyika Marekani ili kulalamikia ubaguzi wa rangi.
Polisi ilitumia maji ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji nje ya maduka makuu katika mji wa kaskazini mashariki wa Recife.
Maandamano hayo yalichochewa kufuatia video iliyosambazwa mitandaoni inayoonyesha walinzi wa duka kuu la Carrefour wakimshambulia mwanamume mweusi Joao Alberto Silveira.
Walinzi hao wamekamatwa na huenda wakakabiliwa na kosa la mauaji.