MAJALIWA Kassim Majaliwa, ambaye amethibitishwa leo Alhamisi, Novemba 12, 2020 na Bunge la 12 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea na wadhifa wa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa muhula wa pili, alizaliwa tarehe 22 Desemba mwaka 1960 yaani miaka 60 iliyopita.
Kitaaluma ni mwalimu aliyepata elimu yake ya ualimu katika chuo cha ualimu cha Mtwara mwaka 1991-1993, na baadaye kujiendeleza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Stockholm nchini Sweden.
Kutoka mwaka 1984 mpaka 2006 amehudumu katika nafasi mbalimbali kama mwalimu na kiongozi wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT). Mwaka 2006 Majaliwa aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya na kisha akajitosa kwenye siasa za ushindani mwaka 2010 alipogombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi.
Baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) wakati wa serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Dkt. Jakaya Kikwete.
Majaliwa ameidhinishwa kuwa Waziri Mkuu na Bunge baada ya jina lake kuwasilishwa bungeni na mpambe wa Rais John Magufuli na kupigiwa kura ya ndiyo na wabunge wote 350 waliokuwepo ukumbini. Anatarajiwa kula kiapo hivi karibuni ili kuanza rasmi majukumu yake.
Majaliwa alikuwa Waziri Mkuu katika kipindi chote cha miaka mitano ya kwanza ya utawala wa Magufuli uliokamilika mwezi uliopita. Endapo atadumu katika wadhifa huo kwa kipindi chote cha pili cha rais Magufuli atakuwa Waziri Mkuu wa pili kuhudumu kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.
Fredrick Sumaye, ndiye kiongozi pekee mpaka sasa aliyehudumu kwa miaka 10 mfululizo kama Waziri Mkuu wa Tanzania kutoka mwaka 1995 mpaka 2005 chini ya rais mstaafu hayati Benjamin Mkapa.
Majaliwa alikuwa Waziri Mkuu katika kipindi chote cha miaka mitano ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli uliokamilika mwezi uliopita. Uteuzi wa Majaliwa hii leo haukusthua wengi kama alivyoteuliwa mara ya kwanza miaka mitano iliyopita. Wachambuzi wengi walitarajia Majaliwa kurejea katika nafasi yake, mosi kutokana na kauli ya rais Magufuli na pili kutokana na utendaji wake.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Magufuli alizungumza wakati wa tukio la kuapishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, kwamba viongozi wa serikali hawatakiwi kuwa na hofu ya nafasi zao kwa sababu mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita yalitokana na ufanisi wao pia.
Ingawa alisema kutakuwa na mabadiliko makubwa katika baraza jipya la mawaziri, ni vigumu kutenganisha mafanikio ya utawala wa Awamu ya Tano na utendaji wa Waziri Mkuu. Katika mawaziri wote wa serikali ya Rais Magufuli, Majaliwa – kama kiranja wa mawaziri wengine, ndiye pekee ambaye nafasi yake inafungamanishwa moja kwa moja na Rais katika utendaji.
Majaliwa anatokea kusini mwa Tanzania eneo ambalo mtu wa mwisho kutoka ukanda huo kuwa waziri mkuu alikuwa Mzee Rashid Kawawa aliyekuwa Waziri Mkuu miaka ya mwanzoni ya uhuru. Yeye ni mtu wa 11 kuwa Waziri Mkuu tangu Tanganyika ilipopata uhuru ambapo Waziri Mkuu wa kwanza alikuwa Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Miongoni mwa Majukumu ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa kila siku wa kazi na shughuli za Serikali, atakuwa na madaraka ya kuongoza shughuli za serikali Bungeni.
Atakuwa na madaraka ya kutekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo rais ataagiza yatekelezwe.
Pia Waziri Mkuu atakuwa na madaraka ya kumshauri rais kuhusu uteuzi wa Mawaziri.
Anayo madaraka ya kumshauri rais kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.
Waziri Mkuu huyu ni mpenzi wa mchezo wa mpira wa miguu, na pia amesomea ualimu wa mpira. Katika kipindi cha mwaka 2010-2015 alikuwa Kocha wa timu ya soka inayoundwa na wabunge pamoja na majukumu mengine mengi.