KAMA alivyosema mnajimu maarufu wa nyota Afrika Mashariki na Kati, Alhaj Maalim Hassan Yahya Hussein kuwa, nyota ya staa mpya wa Bongo Fleva, Zuhura Othman Soud ‘Zuchu’ ni kali mno, ndicho kinachotokea kwa sasa.
Habari za ndani zimeeleza kuwa, kwa sasa midume wanapishana nyumbani kwa mrembo huyo na mama yake wakitaka kutoa posa na kumuweka ndani.
BI KHADIJA ATOA TAMKO
Vyanzo vya karibu na Zuchu ambaye ni zao jipya ndani ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), kuna rundo la wanaume ambao wamekuwa wakijitokeza kutaka kumuoa Zuchu, kiasi cha mama yake mzazi ambaye ni Malkia wa Taarab, Khadija Omar Kopa ‘Bi Khadija’ kutoa tamko.
Chanzo kimojawapo kimelifungukia gazeti hili kuwa, Bi Khadija amekuwa akiwaka ile mbaya kwa maelezo kwamba, bado binti yake ni mdogo na ana mipango yake ambayo bado hajaikamilisha.
“Wasubiri kidogo bwana, kwanza bado umri wake ni mdogo na anatafuta maisha kwanza,” ananukuliwa Bi Khadija akitoa tamko juu ya msururu wa wanaume wanaopishana nyumbani kwake wakijidai kutaka kumposa na kumuoa Zuchu.
Chanzo hicho kimeling’ata sikio gazeti hili kwamba, tangu Zuchu awe staa mkubwa Bongo, amekuwa akifuatiliwa na watu mbalimbali hasa wanaume ambao wanajitokeza na kutaka kutoa posa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
ZUCHU AOMBA KUONGEZEWA ULINZI
Imeelezwa kuwa, usumbufu huo wa wanaume, sasa umekuwa ni kero hata kwa Bi Khadija mwenyewe, achilia mbali Zuchu ambaye wakati mwingine anaingiwa na woga hivyo kuomba WCB wamuongezee ulinzi wa mabaunsa ambao sasa ni wanne badala ya wawili wa awali.
“Huwezi kuamini, hata mama yake sasa anabaki mdomo wazi na kushangaa watu wavyomiminika kumpelekea posa.
“Kuna wengine hata hawajuani, lakini ni vile tu wamemuona ameanza kupata umaarufu mkubwa hivyo nao wanajaribu kuanza kujisogeza na wao hata wapate umaarufu hata kidogo.
“Lakini ukweli ni kwamba Bi Khadija hataki kabisa kusikia kitu kama hicho,” anasema mtoa habari wetu huyo.
MSIKIE BI KHADIJA
Baada ya kupata ubuyu huo wa posa za Zuchu kumiminika kama mvua, gazeti hili lilimsaka Bi Khadija Kopa ambaye alipoulizwa kuhusu kupokea posa kutoka kwa wanaume mbalimbali, alisema anashangazwa mno kwani watu wengi wanamuuliza kuhusu mtoto wake kuolewa, jambo ambalo hata yeye haelewi limeanzia wapi kwa kwa sababu mtoto wake bado ni mdogo.
Bi Khadija anasema kuwa, mbali na udogo wa Zuchu, lakini ndiyo kwanza ameanza angalau kutafuta maisha hivyo ni bora wangemuacha afanye maisha yake kwanza, hayo mengine yatafuata baadaye atakapokuwa tayari yeye mwenyewe.
“Unajua sijui kwa nini wanasema kuhusu posa kwa mwanangu kila mara.
“Mimi ningeomba wamuache kwanza afanye kazi yake vizuri na atafute maisha maana hata hivyo mtoto wangu bado ni mdogo.
“Hayo mambo (ya kuolewa) atayakuta wakati wake sahihi ukifika maana ndiyo kwanza anaanza maisha yake,” anasema Bi Khadija Kopa ambaye yeye amedumu kwenye ustaa kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
TUJIKUMBUSHE
Zuchu amesainiswa kwenye Lebo ya Wasafi chini ya mwanamuziki maarufu Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Hata hivyo, mara kadhaa kumekuwa na madai mazito mitandaoni kwamba, huwenda yeye (Zuchu) na bosi wake huyo kuna kitu kinaendelea na kwamba huwenda baadaye wakaungana na kujenga familia, jambo ambalo wote wamekuwa wakilikanusha.
Wakati hayo yakijiri, Zuchu amekuwa akikanusha kuwa na mwanaume ambapo amekuwa akijibu kwa kifupi; “Nipo single (akimaanisha hana mpenzi).”