Serikali mkoani Shinyanga imekamilisha ukarabati wa jengo la watoto wachanga la hospitali ya Mji wa Kahama lenye thamani ya shilingi millioni 103 pamoja na kuweka vifaa kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti na ICU ya watoto wanaohitaji uangalizi maalum.
Akiongea wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa Majengo hayo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile, alisema kuwa ukarabati wa jengo la watoto wachanga umekamilika na vifaa tayari vimekabidhiwa kwa ajili ya kupangwa na kuanza kufanya kazi na kuongeza kuwa ujenzi wa majengo ya upasuaji uko katika hutua za mwisho kukamilika.
Ufadhili wa fedha za ukarabati wa jengo hilo umetolewa na Shirika la Kimataifa la Touch Foundation ambalo pia linafadhili ujenzi wa Majengo ya upasuaji katika Hospitali ya wilaya ya Kishapu, Kituo cha Afya Lunguya na Burungwa vyote vya Halmashauri ya Ushetu na Msalala, wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Ujenzi wa Jengo la Upasuaji ukiendelea katika hatua za Mwisho jengo hili liko katika Hospitali ya Jakaya Kikwete iliyoko Kishapu Mkoani Shinyanga.
Aidha kwa upande wake Muhandisi wa mkoa wa Shinyanga, Francis Magoti, aliongeza kuwa jengo la watoto wachanga la hospitali ya Mji Kahama hapo awali lilikuwa limechakaa sana, ila baada ya kukarabati na shirika hilo kumeongeza wodi ya watoto njiti na wodi ya uangalizi maalumu ya watoto wagonjwa (ICU).