JONAS Mkude, kiungo mkabaji ndani ya Klabu ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu Sven Vandenbroeck, amesema kuwa vipigo viwili walivyopata kwenye mechi zao za ligi kuliwavuruga kwani walijipanga kupata ushindi.
Simba imeweka rekodi kwa kuwa timu ya kwanza kupokea vichapo viwili mfululizo kwa timu zilizo ndani ya tatu bora msimu wa 2020/21, ambapo kabla ya mechi ya jana ya Yanga dhidi ya Gwambina, Azam ilikuwa nafasi ya kwanza na pointi 22, sawa na Yanga iliyo nafasi ya pili.
Ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake 16, Simba ilipoteza mbele ya Tanzania Prisons kwa kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Nelson Mandela, kisha ikapoteza mbele ya Ruvu Shooting kwa kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Uhuru.Mkude alisema kuwa kupoteza mechi zao mbili kuliwavuruga kwa kuwa hawakufikiria ingeweza kutokea hali hiyo.
“Kiukweli kuhusu kupoteza mechi mbili mfululizo ndani ya ligi sijui nielezeje maana kulituvuruga, hatukupanga kupoteza ila matokeo ndani ya uwanja yalikuwa yanashangaza, sasa yaliyopita tunaachana nayo tunatazama mechi zetu zijazo,” alisema.