MKURUGENZI wa kampuni ya Utalii ya Shidolya ya jijini Arusha, Lazarus Mafie maarufu kwa jina la Shidolya(60)Mkazi wa Kimandolu, wilayani Arumeru, mkoani hapa amefikishwa Mahakamani akituhumiwa kutenda kosa la mauaji ya kukusudia kwa mfanyakazi wake.
Mafie na wenzake wawili wanadaiwa kumuua, Furanael Mbise ambaye alikuwa mlinzi nyumbani kwa Shidolya kwa kumkata na kitu chenye ncha kali na kisha kudanganya kuwa marehemu ameuawa na majambazi.
Akisoma shtaka hilo, mbele ya hakimu Gwanta Mwankuga wa mahakama ya wilaya ya Arumeru na mwendesha mashtaka wa serikali, Naomi Mollel aliiambia mahakama hiyo kwamba mshtakiwa huyo na wenzake wawili walitenda kosa hilo, Oktoba 18 mwaka huu 2020 nyumbani kwa mtuhumiwa.
Mwendesha mashtaka huyo aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Mfanyabiashara, Joseph Mafie(45) Mkazi wa Usa River na Joachim Mwanakatwe au Baraka(26) ambaye ni mtunza bustani wa kampuni ya Shidolya na Mkazi wa Kimandolu wilayani Arumeru.
Watuhumiwa hao kwa pamoja hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na shauri hilo namba 22/2020 kuwa la mauaji na hivyo mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Watuhumiwa hao mara baada ya kusomewa shitaka, walipelekwa mahabusu katika gereza kuu la Arusha lililopo kisongo wilaya ya Arumeru kutokana na shauri hilo kutokuwa na dhamana hadi kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo Desemba 2/2020.
Mwili wa Marehemu Mbise uliokuwa umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika hospital ya mkoa Mount Meru, umezikwa nyumbani kwake huku mtuhumiwa Shidolya akisimamia mazishi hayo ikiwemo kununua jeneza kabla ya kukamatwa na polisi akituhumiwa kuhusika na kifo cha marehemu ambaye alikuwa ndugu yake na alimwajiri kwa shughuli za ulinzi nyumbani kwake.
Katika hatua nyingine kumkuwepo jitihada zanazofanywa na ndugu wasl watuhumiwa ikiwemo mke wa mkurugenzi huyo kuhakikisha wanawanasua na masahibu hao ili kurejea uraiani kinyume cha sheria.