KIUNGO wa Young Africans SC ya Dar es Salaam, Mukoko Tonombe, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba msimu wa 2020/21 huku Cedric Kaze pia wa timu hiyo akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Mukoko na Kaze walitwaa tuzo hizo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mwezi huo wa Oktoba, Yanga ilicheza michezo minne, ikiwa ndiyo timu iliyoshinda michezo yake yote na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha timu 18.
Yanga ilizifunga Coastal Union 3-0, Polisi Tanzania 1-0, KMC 1-2 na Biashara United, 0-1 ambapo Mukoko alitoa mchango mkubwa katika ushindi huo ikiwa ni pamoja na kufunga bao moja dhidi ya Polisi Tanzania.
Kwa upande wa Kaze aliwashinda Aristica Cioaba wa Azam na Francis Baraza wa Biashara United ambapo Kaze aliiongoza Yanga katika michezo mitatu na kushinda yote. Yanga chini ya Kaze ilizifunga Polisi Tanzania, KMC na Biashara United na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili.