Jeshi la Polisi mkoani Morogoro , linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Msingi Montfort iliyoko Kola B, Manispaa ya Morogoro, Eneza Anderson (27), mkazi wa Kihonda Maghorofani kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wake wa darasa la tano.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, tukio hilo liliripotiwa polisi Novemba 5, mwaka huu, majira ya saa 6:00 mchana.
Mutafungwa alisema mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa alimbaka mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 10 (jina linahifadhiwa).
Kamanda Mutafungwa alisema mwanafunzi huyo alipohojiwa alidai kuingiliwa kimwili na mwalimu wake mara kadhaa kwenye maeneo ya ofisini na chooni wakati wanafunzi wenzake wanapokuwa darasani.
Alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka katika ofisi za dawati la jinsia na watoto mkoani Morogoro, mtuhumiwa huyo ni mwalimu wa taaluma katika shule hiyo.
Mutafungwa alisema Jeshi la Polisi lilimhoji mtuhumiwa huyo katika hatua ya awali na kukiri kumbaka na kumlawiti mwanafunzi mara tano.
Kamanda Mutafungwa alisema hatua za kumfikisha mahakamani kwa kushirikiana na maofisa ustawi wa jamii zitafuata baada ya upelelezi kukamilika.