Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr amewaamuru waendesha mashitaka wa serikali kuanzisha uchunguzi kuhusu dosari za upigaji kura, kwa sababu Rais Donald Trump amedai kuwa alishindwa uchaguzi kutokana na udanganyifu.
Barr, ambaye ni mtetezi wa karibu wa Trump kwa muda mrefu, amesisitiza barua yake kwa wanasheria wa Marekani kote nchini sio ishara ya kuwa Wizara ya Sheria ina ushahidi kwa sasa wa matukio halali ya udanganyifu.
Uchunguzi wa udanganyifu katika upigaji kura kawaida hufanywa na majimbo binafsi, ambayo huweka na kuchunguza kanuni zao za uchaguzi.
Amri ya Barr imekuja wakati Trump akipambana kuubatilisha ushindi mwembamba wa mpinzani wake wa Democratic Joe Biden katika majimbo kadhaa muhimu -- Pennsylvania, Nevada, Georgia, na Arizona -- ambayo yalimpa Biden idadi ya kutosha ya kura za wajumbe ili kushinda uchaguzi wa rais kwa ujumla.