KATIKA kile kinachoonekana kumjaribu Rais Dk John Magufuli, Mwenyekiti wa Kijiji wilayani Magu Mkoa wa Mwanza, Badri Juma Masengo (40), anadaiwa kumtundika mimba denti wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa).
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli alieleza kusikitishwa na kitendo cha ‘mafataki’ kukatisha ndoto za wanafunzi wa kike.
Aliongeza kuwa, katika wilaya hiyo yapo mambo ya ovyo yanayofanywa na baadhi ya walimu, wazazi na jamii kwa kufanya ngono na wanafunzi wa shule na kuonya hatakubali hayo yaendelee.
Alitoa angalizo kwa watumishi wa idara ya Polisi na mahakama wanaopindisha sheria kwa sababu ya rushwa kwenye kadhia hiyo hawatabaki salama.
“Rais Magufuli amefuta ada kwa shule za msingi hadi kidato cha nne na kurahisha mambo kwa wananchi ambao hawakuwa na uwezo ili kuwawezesha watoto kusoma kwa raha watimize ndoto zao, lakini watu wachache kwa tamaa ya ngono wanawaharibia maisha.
“Sitawavumilia wanaume wanaojamiiana na watoto na nitoe rai kwa idara ya mahakama na Polisi watende haki kwa mtoto aliyekatishwa masomo,” alisema.
Aidha, mwanafunzi huyo alieleza kuwa ana ujauzito wa miezi miwili na wiki moja.
Alisema kwa muda mrefu mtuhumiwa huyo mtuhumiwa alikuwa akimtongoza ambapo alimfuata nyumbani kwao muda wa saa 6:00 usiku baada ya wazazi wake kwenda msibani na kumwacha na wadogo zake na kumshawishi kuondoka naye hadi kwake.
Alisema walipofika nyumbani hapo mtuhumiwa huyo alimvua nguo kisha akampatia shilingi 20,000 na kumuingilia, lakini hata hivyo, baada ya kutimiza haja zake alimnyang’anya fedha hizo na kumrejesha tena kwao usiku huo huku akimpa ahadi ya kumpa matumizi na nguo, lakini hakutimiza ahadi hiyo.
Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Magu, Glory Vicent Mtui amemshukuru mkuu huyo wa wilaya hiyo kwa jinsi anavyoshughulikia changamoto ya mimba kuhakikisha wahusika wanakamtwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kata Kahangara, John Clavery Mabati alisema kuwa, mtuhumiwa alipokamatwa na kuhojiwa alikiri kufanya ngono na kumpa ujauzito mwanafunzi huyo.
Alisema Jeshi la Polisi Wilaya ya Magu linaendelea kumshikilia mwenyekiti huyo kwa mahojiano kutokana na kutenda kosa hilo kabla ya kufikishwa mahakamani.
Mwalimu mkuu wa shule anayosoma mwanafunzi huyo alisema mwanafunzi huyo ambaye alikuwa miongoni mwa 10 waliopelekwa kwenye vipimo vya mimba, alibainika kuwa na ujauzito na hakuwahi kuwaeleza wazazi kitendo alichofanyiwa.