Pemba. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba limefanikiwa kuupata mwili wa aliyekuwa askari wa kikosi cha KVZ Khalfan Junedi aliyedaiwa kuuawa wiki tatu zilizopita eneo la Ngwachani Wilaya ya Mkoani.
Pamoja na mwili huo jeshi hilo pia limefanikiwa kuipata bunduki aina ya AK47 katika eneo la Ngwachani Novemba 12 majira ya saa 2:00 usiku huku magazine yake ikiwa na risasi 21.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Ahmed Khamis Makarani amesema mwili huo ulipatika katika kijiji cha Chonga kwenye bonde la Kisitu mbwa.
Alisema kuwa, Novemba 15 walifanikiwa kuupata mwili wa askari huyo baada ya kumkamata mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Ussi Foum Machano mkazi wa Ngwachani, ambaye aliwapeleka kwenye eneo alilofukiwa.
“Novemba 12 tulimkamata Ussi, maeneo ya Chake Chake, tulimhoji na ndipo akatuambia mahala ilipo bunduki na baadaye kwenda kutuonyesha eneo alipowekwa marehemu huyo”, amesema Kamanda Makarani.
Ameeleza kuwa, baada ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi, walibaini kuwa marehemu kabla ya kifo chake alikuwa na majeraha ya kupigwa huku akiwa amekatwa baadhi ya viungo vya mwili wake.
“Taratibu zote za kiuchunguzi kuhusiana na mwili zimefanywa, mwili umesafirishwa kwenda Unguja kwa ajili ya mazishi”, amesema.
Alisema kuwa, upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika na kusema kuwa wanaamini watawakamata watu wengine waliohusika na tukio hilo.
Amesema kuwa, Oktoba 28 mwa huu askari huyo pamoja na wengine walikuwa kwenye doria za kawaida, ambapo askari huyo alipotea majira ya saa 2:00 usiku akiwa na bunduki AK47.
Aidha, kamanda Makarani amewataka wananchi wa Ngwachani kurudi katika maeneo yao ya kuishi, ili waendelee na shughuli zao za maisha, kwani amani na utulivu imerejea.
“Waliokuwapo maporini warudi na waliokuwa nje ya Pemba warudi, sisi kimsingi tunawatafuta watu ambao kwa namna moja ama nyingine wamehusika na mauaji ya huyo askari na sio wananchi wa kawaida”, amesema.