Mwinyi Amkaribisha Maalim Seif Kufanya Maridhiano


RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema yuko tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa, kuendesha serikali kama ambavyo Katiba ya Zanzibar inavyoelekeza. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne tarehe 11 Novemba 2020 wakati akizindua Baraza la 10 la Wawakilishi Zanzibar.


Mwinyi ambaye ni rais wa nane wa Zanzibar, aliingia madarakani tarehe 2 Novemba, 2020, akipokea kiti kilichoachwa na Dk. Ali Mohamed Shein aliyemaliza muhula wake wa miaka kumi ya uongozi.


Pia ametoa pongeza kwa wajumbe wa baraza hilo kwa kuaminiwa na wananchi akiwemo yeye mwenyewe kwa kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020.


Katika uchaguzi huo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ilimtangaza  Mwinyi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mshindi kwa kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote 382,402.  Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo alipata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.


Mwinyi amesema, wananchi “wametuchagua kwa sababu tuna kiu ya kutimiza matarajio yao na heshima yetu itatokana na sisi kutimiza ahadi zetu, maana si tu ahadi bali kutimiza deni ni kulinda heshima.”


“Niwahakikishie, dhamira yangu na  serikali nitakayoiunda ni kutimiza matakwa ya wananchi wetu,” amesema  Mwinyi ambaye ni mtoto wa rais mstaafu wa Tanzania na Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi.




Huku akishangiliwa na wajumbe wa baraza hilo,  amesema “kura nyingi tulizopigiwa na wananchi ni ishara ya matumaini makubwa ya wananchi kwa chama chetu na kwangu mimi binafsi na ni wajibu wetu sasa kukidhi matarajio ya wengi.”




Ametumia fursa hiyo, kuvishukuru vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi na kuyapokea matokeo na kuheshimu uamuzi wa wananchi.




“Ninaheshimu maridhiano na matakwa ya katiba ya kushirikiana na vyama vingimne vya siasa katika kuendesha serikali na niko tayari kuyatekeleza maridhano kama katiba ya Zanzibar inavyoeleza,” amesema.




Katiba ya Zanzibar inaelekeza, Serikali ya Umoja wa Kitaifa itaundwa na chama tawala na chama kilichoshika nafasi ya pili ambapo kutakuwa na makamu wawili wa rais.


Makamu wa kwanza wa rais, atatokana na chama kilichoshika nafasi ya pili na makamu wa pili atatokana na chama kilichoshinda urais. Pia, baraza la mawaziri litahusisha vyama hivyo.


Kwa maana hiyo, katika matokeo ya uchaguzi mkuu, chama ambacho kinakidhi matakwa ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni chama cha ACT-Wazalendo. Hivi karibuni, ACT-Wazalendo wakizungumza na MwanaHALISI Online walisema watakutana kama chama ili kuajdili na kufikia mwafaka wa ama kukubali kushirikiana na serikali itakayoundwa na Rais Mwinyi au vinginevyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad