JESHI la Polisi Mkoani Tabora linamshikilia Mzee wa miaka 67 kwa tuhuma za unyanyasi wa kijinsia na kusababisha ujauzito kwa mtoto wa miaka 13 ambaye ni mjukuu wake.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora ACP Barnabas Mwakalukwa wakati wa mkutano na waandishi wa Habari.
Alisema mnamo tarehe 13 Mwezi huu mama mzazi wa mtoto huyo aligundua kuwa mtoto wake anayesoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Kizigo iliyopo Manispaa ya Tabora (jina linahifadhiwa ) ni mjamzito.
Kamanda alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Said Tumaini ambaye ni Mganga wa Kienyeji na Mkazi wa Kizigo katika Manispaa ya Tabora.
Katika tukio jingine Jeshi limefanikiwa kukamata vitu mbalimbali ambavyo vinadhaniwa kuwa ni vya wizi baada ya watu waliokuwa wamevipakia katika pikipiki tatu kuviacha na kukimbia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Mwakalukwa alivitaja vitu vilivyokamatwa ni pamoja Runinga tatu, Komputya, Friji , Redio za Muziki(sabufa) tano na spika zake , pikipiki tatu zenye usajili wa MC 545 AGZ , MC 224 AXL na nyingine ambayo haina namba.
Alisema msako dhidi ya watu hao waliotoroka na kuacha pikipiki hizo na vitu hivyo unaendelea na kuwataka watu wenye taarifa ya watu hao kutoa taarifa Polisi.
Mwakalukwa alisema watafanyia uchunguzi wa kubaini hizo pikipiki ni mali ya nani na kutoa wito kwa wahusika kujisalimisha wenyewe kabla hajakamatwa.
Wakati huo huo Polisi imefanikiwa kumkamata Joyce Seth wenye umeri wa 52 na Emmanuel Shayo wenye miaka 42 wote wakazi wa Kiloleni Mkoani Tabora wakiwa na mtambo mmoja na lita 120 za Pombe haramu ya gongo.
Alisema watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani mara baada ya taratibu kukamilika.
Kamanda Makalukwa alisema Jeshi la Polisi linaendelea na misako mikali dhidi ya waharifu na watu wote watakaokutwa wakizurura nyakati za usiku wa kuanzia saa 6 watakamatwa.
Aidha aliwataka vijana kutumia msimu huu wa masika kulima mazao mbalimbali na kuachana na kutafuta fedha kwa njia ya kihalifu.