DAR: Kwa harakaharaka unaweza kusema kwa mwaka huu wa 2020 unaoelekea ukingoni, mwanadada Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’, ameua ndege wawili kwa jiwe moja; alifanikisha kolabo na mastaa wakubwa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ na Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’.
Baada ya kukamilisha hilo, Gazeti la IJUMAA lina habari za ndani mno zinazodai kwamba, sasa Nandy anadaiwa kufanya jaribio la kumpindua mwanadada mwingine wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’ kutoka mikononi mwa bosi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Imeelezwa na watu wa karibu kwamba, lengo la Nandy au The African Princess kufanya hivyo ni ili kufanikisha ndoto yake ya kufanya kolabo na Diamond au Mondi, lakini anaona kama Zuchu anamuwekea kauzibe.
NANDY AMEFANYA VIZURI
Hata hivyo, watu wa karibu wa Nandy wanaamini kwamba ndiye msanii wa kike aliyefanya vizuri zaidi kuliko wengine kwa sababu ya nyimbo zake ‘ku-trend’ kwenye chati mbalimbali za muziki ndani na nje ya Bongo, lakini anahitaji kutikisa kwa mara nyingine akiwa na Mondi.
Mbali na hilo, pia amelamba madili ya kutosha kuliko msanii mwingine yeyote wa kike nchini.
Imeelezwa kwamba, Nandy ameweza kutoa nyimbo tano ambazo ni Na Nusu, Acha Lizame akiwa na Harmonize au Harmo, Dozi, Do Me akiwa na mchumba’ke, William Lymo ‘Billnass’ kisha akamalizia na Nibakishie akiwa na King Kiba na nyimbo zote hizo zimefanya vizuri kwenye chati za muziki.
“Ukweli ni kwamba namba huwa hazidanganyi. Kwa mfano video ya wimbo wake wa Na Nusu una zaidi ya watazamaji milioni 2 pale mjini YouTube, Video ya Acha Lizame ina zaidi ya watazamaji milioni 6, Video ya Dozi inakaribia watazamaji milioni moja na Video ya Do Me inakaribia watazamaji milioni.
HIYO NGOMA NA SIMBA ITAKUWAJE?
Sasa hiyo Video ya Nibakishie ndiyo hatari na nusu maana ndani ya siku chache tu inakaribia watazamaji zaidi ya milioni 2. Sasa fikiria hiyo ngoma atakayofanya na Simba (Mondi) itakuwaje? Ngoja tuone.
INABIDI AMTOE ZUCHU KWANZA
“Unajua Nandy amefanya kazi na wasanii wakubwa hapa nchini Tanzania ambao ni Harmonize na Kiba sasa amebakisha huyo Simba pekee kwa hiyo nguvu zote ameelekezea huko, lakini inabidi amtoe Zuchu kwanza ndipo azame kirahisi.
“Kibiashara inaweza kuwa nzuri kwa upande wake kwani anaweza kuongeza wengi mashabiki wapya kutoka kwa Simba (Mondi) ambaye ana nguvu kubwa ya mashabiki mtaani na mitandaoni,” kilimalizia chanzo chetu imara.
NDANI YA UONGOZI WAKE
Mtu mmoja ndani ya uongozi wa Nandy aliliambia Gazeti la IJUMAA kuwa, uongozi wake huo, unataka kumpaisha zaidi baada ya kufanya kazi na Harmo kisha King Kiba na sasa anaweza kufanya ngoma kali na Mondi na watu wakashangaa.
“Yaani asikuambie mtu, uongozi wa Nandy una mikakati mizito sana, utawashangaza watu wengi kwa sababu una mpango kabambe juu ya kolabo ya Nandy na Diamond na watalikamilisha hilo hivi karibuni,” alisema mtu huyo kwa sharti la kutotajwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa Nandy.
KUZIZIDI NGOMA ZA ZUCHU NA MONDI
Mtu huyo aliendelea kufunguka kuwa, ngoma hiyo itakuwa kali mno kiasi cha kuzizidi zile za Zuchu na Diamond (Cheche na Litawachoma) na lengo ni kuzifanya kusahaulika kabisa.
Mtu huyo anasema kuwa, labda tu uongozi wa Wasafi Classic Baby (WCB) uweke ngumu, jambo ambalo hawalitarajii kwa sababu Nandy hana tatizo na Wasafi.
KUMTENGENEZA KIMATAIFA ZAIDI
Pia mbali na hayo yote, lakini inaelezwa kwamba uongozi wake unataka kumtengeneza kimataifa zaidi ndiyo maana wanamuziki wote wakubwa atafanya nao kazi na hata nje ya nchi.
NANDY NA IJUMAA
Baada ya kuinyaka ishu hiyo, Gazeti la IJUMAA lilizungumza na Nandy ambapo lilimuuliza kuhusu hilo.
Nandy anasema kuwa, kila kitu anapangiwa na uongozi wake hivyo yeye anaambiwa tu.
“Mimi jamani kila kitu ni juu ya uongozi wangu na si mimi kama mimi hivyo wakiniambia nifanye kolabo na na Diamond, ni sawa na yeyote yule maana wao ndiyo wananipangia,” anasema Nandy akiomba kutolizungumzia hilo kiundani.
NANDY, ZUCHU NA MONDI
Hivi karibuni, wasanii hawa watatu ndiyo pekee walioibuka kidedea kwenye tuzo kubwa zinazofanyika kila mwaka barani Afrika ambazo ni Tuzo za AFRIMMA.