Chama cha NCCR Mageuzi, kupitia kwa Mwenyekiti wake James Mbatia, kimewataka wananchi kuunga mkono juhudi zao za kutafuta muafaka wa kitaifa ili kulinda maadili na misingi ya taifa.
Mbatia amesema wameamua kuja na mpango huo ambao pia upo kwenye Ilani yao, kutokana na kutoridhishwa na uchaguzi, hivyo moja ya vitu watakavyodai ni kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi.
''NCCR Mageuzi inahimiza maridhiano ya kitaifa kupitia muafaka wa kitaifa ambao utakubaliwa na wananchi wote kwa pamoja kuhusu kuheshimu na kulinda maadili na misingi ya taifa letu, na huko ndipo tutapata tume huru ya uchaguzi'' - James Mbatia
Aidha Mbatia ameongeza kuwa ''Sisi NCCR Mageuzi tumetafakari na kukubaliana kuwa utajiri wetu ni asili yetu na sisi tuna Ilani yetu ambayo agenda namba moja kwenye ilani yetu ya uchaguzi ni Muafaka wa Kitaifa''.
Kwa upande mwingine Mbatia amefafanua kuwa ''Tunahitaji muafaka wa Kitaifa kwa sababu sisi NCCR Mageuzi tumebaini ubaguzi wa ndani ya taifa ndio unaotuumiza zaidi kuliko ule wa kutoka mataifa mengine''.