POLISI katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, wamemkamata mwanamme mwenye umri wa miaka 54, aliyeligongesha gari lake katika lango la ofisi ya Kansela wa nchi hiyo, Angela Merkel, asubuhi ya leo.
Gari hilo dogo la rangi ya bluu lilikuwa na maandishi meupe yenye ujumbe wa kisiasa. Baadhi ya ujumbe huo ulisema, ”simamisheni siasa za utandawazi”.
Taarifa ya polisi imesema maafisa wamemkamata haraka mwanamme huyo na kumweka kizuizini, na uchunguzi unafanyika kubainisha ikiwa hicho kilikuwa kitendo cha kudhamiria.
Wakati wa tukio hilo Kansela Merkel alikuwa akiongoza kikao cha baraza la mawaziri, na msemaji wake amearifu kuwa mkutano huo haukuwa chini ya kitisho chochote cha usalama.
Vyombo vya habari vimearifu kuwa gari hilo hilo lilitumiwa katika kisa kingine kama hicho mwaka 2014 mahali hapohapo, wakati huo likiwa na ujumbe wa kuonyesha hatari ya mabadiliko ya tabianchi.