Kwa siku za usoni kumekuwa na matukio mengi ya majanga ya moto. Matukio haya husababisha uharibifu mkubwa wa mali au hata kugharimu maisha ya watu.
Kwa hakika kuunguliwa na nyumba au mali zako unazozipenda ni jambo baya ambalo usingependa litokee.
Kutokana na mazingira na miundombinu duni ya majengo, majanga ya moto yameendelea kuwakumba watu wengi. Hata hivyo zipo njia kadhaa unazoweza kutumia kukabili majanga ya moto.
Karibu ufuatilie makala hii ili nikushirikishe njia 10 za kuepuka majanga ya moto kwenye nyumba pamoja na tahadhari unazoweza kuchukua.
1. Tumia mfumo bora na salama wa umeme
Majanga mengi ya moto husababishwa na hitilafu zinazotokana na mifumo duni ya umeme.
Kutokana na ukosefu wa elimu au uhaba wa pesa, watu wengi hutumia vifaa duni wakati wa kuweka umeme kwenye nyumba. Mambo ya kuzingatia ili kuwa na mfumo bora wa umeme:
Tumia vifaa bora vya kuwekea umeme kwenye majengo. Epuka mambo kama vile matumizi ya nyaya laini za spika au kuunganisha nyaya kwa kutumia nailoni; hivi huweza kusababisha moto.
Epuka kuhamisha umeme kutoka kwenye nyumba moja hadi nyingine bila kutumia vifaa sahihi.
Tumia mtaalamu, yaani fundi anayefahamu vyema taaluma ya umeme. Ukimtumia mtu asiye na ujuzi wa kutosha atakuwekea mfumo duni unaoweza kusababisha moto.
2. Tumia soketi na swichi vyema
Kutokana na ujenzi duni, si jambo la kustajabisha kukuta nyumba moja ina soketi moja au mbili. Hili husababisha watu kujaza kila kifaa kwenye soketi hiyo moja, swala ambalo hufanya soketi hiyo izidiwe na kuwaka moto.
Hakikisha huweki mzigo mkubwa kwenye soketi au kebo ili kuzuia hatari ya kutokea kwa moto. Pia hakikisha watoto hawachezei soketi au swichi za umeme.
3. Tumia jiko vyema
Ikiwa una jiko lililoko ndani ya nyumba unatakiwa kuchukua tahadhari zaidi. Haijalishi ni jiko la umeme, gesi au mafuta unatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo ili kuepuka majanga ya moto.
Usiwashe jiko ikiwa hakuna mtu karibu.
Usiache watoto wachezee au watumie jiko bila uangalizi wa karibu.
Epuka matumizi ya jiko la mkaa au kuni ndani ya nyumba. Hili limekuwa ni chanzo kikubwa cha moto.
Tumia jiko bora. Kwa mfano kutumia jiko la gesi linalovuja gesi kunaweza kusababisha mlipuko.
Safisha jiko lako vyema. Kuacha jiko likiwa na mafuta au kuacha makaratasi karibu na jiko kunaweza kusababisha moto.
4. Usiache moto ukiwaka karibu na nyumba
Kuna wakati mtu anawasha moto karibu na nyumba. Kuwasha moto karibu na nyumba kunahitaji tahadhari kubwa kwani kunaweza kusababisha janga la moto.
Kumbuka upepo unaweza kusababisha moto kukutana na nyumba, hivyo ni muhimu kuhakikisha unazima kila moto unaouwasha nje ya nyumba.
5. Tumia moto ulio wazi kwa uangalifu
Mara nyingine watu wanawasha vibatari, mishumaa au hata sigara ndani ya nyumba. Vitu hivi vinaweza kusababisha janga kubwa la moto ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa. Unaweza kuzingatia haya:
Usiwashe kibatari au mshumaa wakati hakuna mtu karibu.
Usiruhusu watoto wachezee au watumie kibatari na mshumaa ndani ya nyumba.
Usiweke kibatari au mshumaa karibu na vitu vinavyoweza kushika moto.
Usiache kitu chochote kikiwaka wakati uko usingizini kwani lolote linaweza kutokea.
Usivute sigara ndani ya nyumba.
6. Andaa miundombinu na vikabili moto
Ni vyema kuchukua tahadhari kabla ya janga kutokea. Ni muhimu ukahakikisha nyumba yako ina miundombinu ya kukabili moto pamoja na vifaa ya kuzimia moto. Unaweza kufanya haya yafuatayo:
Weka vifaa vya kuhisi moto au moshi (smoke detectors).
Hakikisha watu wanaweza kujiokoa kwa kupitia madirishani au kwenye milango ikiwa moto utatokea. Yaani jenga madirisha na milango inayoruhusu watu kujiokoa.
Weka vifa vya kuzimia moto kama vile mpira wa maji wa kuzimia moto pamoja na mitungi ya hewa.
7. Tumia vifaa vya umeme vyenye ubora
Katika hoja ya kwanza nilieleza juu ya kutumia mfumo bora wa umeme kwenye nyumba; na hapa ninaeleza umuhimu wa kutumia vifaa bora vya umeme kwenye nyumba.
Ni muhimu kuhakikisha vifaa kama vile redio, pasi, jokofu, televisheni, jiko, n.k. vina ubora unaotakiwa ili kuzuia vifaa hivyo kushika moto.
8. Epuka vitu vinavyoshika moto haraka
Kuna vitu vinavyoshika moto haraka, vitu hivi ni hatari kuwekwa kwenye nyumba; vitu hivi ni kama vile mafuta ya magari au taa, rangi, gesi, pamba, n.k. Hakikisha unachunguza kila bidhaa unayotaka kuiweka kwenye nyumba yako ili kubaini kama inashika moto haraka ili ihifadhiwe kwa tahadhari kubwa.
9. Chukua tahadhari umeme unapokatika
Umeme wa nchi nyingi za Afrika hauaminiki sana, unakatika mara kwa mara na huwa na viwango tofautitofauti. Kwa kiasi kikubwa swala hili limechangia kutokea kwa majanga mengi ya moto.
Hata hivyo kuna tahadhari kadhaa unazoweza kuzichukua kukabiliana na tatizo hili.
Zima vifaa vya umeme mara umeme unapokatika. Mara nyingi umeme hurudi kwa kiwango kikubwa na unaweza kusababisha vifaa vyako kushika moto.
Tumia vifaa vya kutawala kiwango cha umeme (Automatic Voltage Regulator – AVR pamoja na Stabilizer). Vifaa hivi huhakikisha umeme unaoingia kwenye vifaa vyako ni wa kiwango kinachotakiwa. Pia vifaa hivi huwa na mfumo unaojulikana kama “delay” ambao hauruhusu umeme kuingia kwenye vifaa moja kwa moja mara unaporudi.
10. Elimu sahihi kwa wanafamilia
Elimu sahihi ni msingi mkubwa wa kuepuka matatizo. Ni muhimu kuhakikisha kila mwanafamilia au mkazi wa nyumba husika anafahamu tahadhari za kiusalama za kujikinga na majanga ya moto.
Kwa njia hii ya kupata elimu na maarifa stahiki kila mtu atakuwa mwangalizi na mlinzi wa usalama wa nyumba dhidi ya majanga ya moto.
#ZINGATIA
Pamoja na njia hizi kadhaa zilizoelezwa hapa juu ya kujikinga na majanga yamoto, kuna jambo moja unalotakiwa kuchukua tahadhari.
Ni muhimu kuhakikisha nyaraka au vitu vya thamani kubwa vinahifadhiwa mahali salama ambapo haviwezi kuungua kwa moto. Nimeshuhudia watu wakipoteza vyeti, hati muhimu pamoja na pesa kutokana na kutokuvihifadhi mahali salama.
Neno la Mwisho
Kwa hakika majanga ya moto yanaepukika kwa kiasi kikubwa ikiwa utachukua tahadhari sahihi. Ni muhimu kuhakikisha usalama wa nyumba na vifaa vyako ili kuepuka kupata hasara kubwa kwenye maisha yako.