Na Amiri Klagalila,Njombe
Club ya Njombe imewaadhibu bao 2-0 timu ya Lipuli Fc ya mkoani Iringa katika mchezo wao wa ligi daraja la kwanza uliochezwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Amani uliopo mjini Makambako na kufanikiwa kutoka na point tatu mkononi na kuwa na jumla ya point 6 .
Njombe mji waliokuwa nafasi ya 8 sasa wanapanda na kuwa nafasi ya 6 ikiwa ni mchezo wao wa kwanza kucheza uwanja wao wa Nyumbani huku wapinzani wao Lipuli wakisalia nafasi ya 2 kwa kuwa na point 10 kibindoni.
Mwenyekiti wa timu ya Njombe mji Bwana,Senetor Mwaikambo amepongeza wachezaji wake huku akisema miongoni mwa sababu za ushindi huo ni pamoja na mshikamano wa viongozi wapya wachezaji pamoja na mashabiki wa timu hiyo.
“Siri ya ushindi huu ni mshikamano na toka tumeteuliwa tuna siku kumi kama kamati ya muda na tumejipanga vizuri na malengo yetu sisi ni kuhakikisha timu inatoka ligi daraja la kwanza kwenda ligi kuu”alisema Senetor Mwaikambo
“Tunaomba sapoti kwa wananjombe na waendelee kutuunga mkono ili kuleta mafanikio kwenye timu yao na wawe pamoja na sisi hatuna timu inayoshiriki ligi zaidi ya hii”aliongeza Mwaikambo
Kocha msaidizi wa Nombe mji Albert Gama amesema ushindi huo ni kutokana na maandalizi mazuri waliokuwa nayo.
“Matokeo ni mazuri na sisi tulijiandaa kwa hiyo mechi hii maana yake ni maandalizi ya mechi inayokuja na tunaendelea kucheza kwa malengo “alisema Albert Gama
Kwa upande wake kocha wa Lipuli FC Abdul Mingange amesema wanakwenda kurekebisha makosa yao ili kurudi kwenye mchezo kwa kuwa mchezo ulikataa licha ya wao kujipanga na kucheza mchezo mzuri.
Katika mchezo huo mchezaji Notikely Masasi ndiye mchezaji aliyesaidia kwa kiwango kikubwa ushindi wa Njombe mji na kufanikiwa kuifungia timu yake mabao yote mawili.