PLATEAU United ni wapinzani wa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika lakini uongozi wa timu kutoka nchini Nigeria, umesema kuwa tayari umeanza kuwafuatilia kwa karibu wapinzani wao kwa kuwa malengo yao ni kufika mbali baada ya ratiba kutoka.
Simba imepangwa kucheza na timu hiyo katika mchezo wa hatua ya awali uliopangwa kupigwa kati ya Novemba 27 hadi 29, mwaka huu Nigeria kabla ya mchezo wa pili ambao utakuwa wa marudiano utakaopigwa kati ya Desemba 4 hadi 6, mwaka huu kwenye Uwanja Benjamin Mkapa jijini Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkuu wa Idara ya Habari ya timu hiyo, Albert Dakup, alisema kuwa wao wamejipanga tayari kwa michuano hiyo na wameshaanza mipango ya kuwafuatilia kwa karibu wapinzani wao katika michuano hiyo kutokana na kutambua ubora wao.
“Hakuna kitu maalum juu yake kwa sababu ikiwa uko kwenye mashindano, unapaswa kuwa tayari kukabiliana na upinzani wowote. Kama timu tunawaheshimu wapinzani wetu na hatuogopi adui yeyote.
“Lakini tumeanza mikakati ya kuwafuatilia kujua wapi wako bora sana, ingawa siyo timu ambayo inatisha sana katika michuano ya kimataifa, matarajio yetu ni kuweza kupata matokeo mazuri kwao na ndiyo jambo ambalo tunalitegemea, japokuwa haliwezi kuwa rahisi,” alisema Dakup.