Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amepuzilia mbali matokeo ya uchaguzi wa rais wiki iliyopita yalioonyesha kuwa Rais Donald Trump ameshindwa.
Pompeo amewaambia waandishi habari kuwa kipindi cha mpito kuelekea muhula wa pili wa Trump kitatokea bila wasiwasi wowote.
Hata hivyo baadaye alisema wizara ya mambo ya nje itakuwa tayari bila kujali nani atakayekuwa Rais mnamo Januari 20, mwakani.
Kauli ya Pompeo kuashiria kuwa Trump anaweza kuhudumu tena kwa muhula wa pili, inakuja wakati ambapo Trump amekataa kukubali kushindwa na Rais mteule Joe Biden.
Pompeo ambaye ni mwanadiplomasia mkuu wa Marekani ameyasema hayo licha ya viongozi mbalimbali duniani kuendelea kumpongeza Biden kwa ushindi wake.