MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Azam FC, raia wa Zimbabwe, Prince Dube amesema kuwa mipango yake kwa sasa ni kuhakikisha anafunga kwenye kila nafasi atakayoipata kwenye michezo ijayo ikiwemo dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumatano ijayo.
Dube akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe Jumatatu hii alifanikiwa kuifungia timu hiyo bao moja dhidi ya timu ya Algeria katika sare ya mabao 2-2.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Dube alisema: “Naushukuru uongozi wa klabu yangu ya Azam kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakinionyesha tangu nimefika Tanzania, naweza kusema hiyo ni miongoni mwa sababu kubwa zilizonifanya nianze vizuri na kufanikiwa kufunga mabao sita.
“Tunahitaji kushinda michezo hii ili kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuweza kutwaa ubingwa msimu huu. Nami kama mshambuliaji nimejipanga kuhakikisha natumia vizuri nafasi za kufunga kwenye kila mchezo unaokuja ili kuisaidia timu yangu kufikia malengo tuliyojiwekea msimu huu,” alisema Dube.