Rais Andres Manuel Lopez Obrador wa Mexico amesema hawezi kumpongeza mshindi wa urais wa uchaguzi wa Marekani, Joe Biden, mpaka taratibu za kisheria zitakapohitimishwa, akisema msimamo wake huo ni wa busara za kisiasa.
Hapo jana mgombea wa chama cha Democratic, Joe Biden alitangazwa kuwa rais mteule wa Marekani, kufuatia ushindi wake katika jimbo la Pennsylvania ambao ulimfanya apate kura za wajumbe maalum zaidi 270 zinazohitajika.
Rais Trump ameanzisha mchakato wa kisheria kupinga matokeo hayo, ingawa maafisa wa uchaguzi katika majimbo tofauti ya Marekani wanasema hakuna ushahidi wa maana wa udanganyifu na wataalamu wa sheria pia wakisema juhudi za Trump haziwezi kufanikiwa.