NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta atakosekana katika mchezo wa kwanza wa kufuzu AFCON dhidi ya Tunisia kufuatia majeraha aliyoyapata wakati akitumikia klabu yake ya Fenerbahce ya Uturuki.
Samatta amepata majeraha hayo siku ya Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Uturuki dhidi ya klabu ya Konyaspor ambao ulimalizika kwa Fenerbahce kufungwa mabao 2-0.
Akizungumzia majeraha hayo, Samatta amesema kuwa amefanyiwa vipimo anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya siku 10 kwa ajili ya kuipumzisha misuli ili ireje katika hali yake ya kawaida.
“Mechi ya mwisho ya ligi nilipata maumivu ya misuli na nilifanyiwa vipimo na majibu yametoka mabaya natakiwa kuwa nje kwa zaidi ya siku 10. Na ripoti ya inaeleza napaswa kupumzika ili misuli irejee katika hali ya kawaida, imeniumiza sana lakini sina jinsi, nilitamani kuwepo kama kiongozi wa timu. Lakini sina namna ila nimekuja kuongea na vijana na Mwalimu nijue hali yao ikoje,” alisema Samatta.
Mchezo wa kwanza wa timu ya taifa ya Tanzania wa kufuzu AFCON dhidi ya Tunisia utakaochezwa Novemba 13, 2020 mjini Tunis, mchezo wa marudio utachezwa Novemba 17, 2020 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam