SHANGWE, vifijo na nderemo zilitawala jana wakati wa kufanya majaribio ya Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani na nje ya nchi cha Mbezi Luis wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam.
Mabasi manane ya abiria yalitumika kufanya majaribio hayo na kusimamiwa na Ofisi za Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Ubungo na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Wananchi walifurika katika stendi hiyo mapema wakiwa na shauku ya kuona kitakachojiri ambako ilipofika saa 6:30 mchana msafara wa mabasi manane ukiongozwa na askari wa usalama barabarani uliwasili kituoni hapo.
Kelele zilitawala baada ya basi la kwanza kuingia huku kivutio kikubwa kikiwa ni namna mabasi hayo yalivyopangwa na kuachana kwa sekunde 30 kutoka basi moja hadi jingine huku madereva wa wakipiga honi ikiwa ni mwitikio wa salamu zilizokuwa zikimiminwa na wananchi kwa kuwashangilia.
Furaha ilionekana wazi kuwazidi wananchi hao na kuanza kumtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kwa kusema ‘Magufuli Baba lao’ na wengine wakisema ‘Magufuli jembe.’
Mabasi yaliyoingia katika stendi hiyo ni New Force mbili, Abood mbili, Happy Nation mbili, ASK na BM.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana aliridhishwa na majaribio hayo na kuwaambia waandishi wa habari kuwa majaribio hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu lengo lilikuwa kuangalia vipimo vya nafasi za kuegesha basi na uwezo wa basi kugeuka ndani ya stendi hiyo.
“Majaribio yetu mpaka sasa yanakwenda vizuri tumejaribu mabasi yetu katika sehemu za kupakia abiria tumeona zinatosha vizuri, tumewajaribu madereva wetu namna ya kupaki na kutoa gari sehemu za kupakia abiria tumeona wanaweza na hakuna shida yoyote,” alisema Liana.
Alisema kama mambo yatakwenda yalivyopangwa wanatarajia Novemba 30, mwaka huu, kukifungua rasmi kituo hicho na kuhamisha kutoka Kituo cha sasa cha Ubungo.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Ubungo, Ibrahim Samwix aliwaambia wanahabari kuwa usalama katika stendi hiyo kuanzia usalama wa mabasi na abiria na watumiaji wote uko juu na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuendelea kuwashangaza Watanzania kwa maendeleo.
Alisema majaribio yote ya magari na madereva yamekwenda vizuri na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo waliyopewa na Rais Magufuli bila woga wala wasiwasi kwani usalama ni kipaumbele namba moja cha Jeshi la Polisi.
Wakati wa majaribio hayo, abiria wote waliokuwemo katika mabasi hayo walishushwa katika eneo maalumu ikiwa ni moja ya mikakati ya kuhakikisha usalama wao wakati wa kuyafanyia majaribio mabasi yaliyochaguliwa.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili, walisema stendi hiyo ni moja ya matukio ya kihistoria anayoyafanya Rais Magufuli. Waliiomba serikali kuweka utaratibu mzuri ili kituo kiinufaishe serikali na wananchi.
Mkazi wa Kimara Baruti, John Samweli aliwataka Watanzania waiunge mkono serikali katika kuleta maendeleo. “Watanzania tuwe tayari kushirikiana na serikali yetu ili iweze kutekeleza mambo makubwa kama haya,” alisema.