MBUNGE wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, ametajwa kuwa miongoni mwa wanafunzi bora watatu ambao ni wahitimu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO) katika kozi ya Shahada ya Kwanza ya Mawasiliano ya Umma (Bachelor of Arts in Mass Communication) mwaka 2020.
Hafla ya kukabidhiwa vyeti hivyo imefanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Tumaini Kampasi ya Dar es Salaam, jana Ijumaa, Novemba 20, 2020, na kuhudhuriwa na wanafunzi wahitimu wa kozi mbalimbali chuoni hapo, wanafunzi wanaoendelea na masomo, wahadhiri na wahadhiri wasaidizi na jumuiya ya chuo kikuu hicho.
Shigongo ambaye hajawahi kusoma elimu ya sekondari, alijiunga na chuo kikuu hicho kupitia mfumo wa mitihani ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) uitwao Recognition of Prior Learning (RPL) kutokana na kipaji cha mtu na mchango wake katika tasnia husika. Baada ya kufanya mitihani hiyo mwaka 2017 alifaulu vizuri kwa kupata Daraja A ndipo akapewa kibali na TCU cha kujiunga na masomo ya chuo kikuu.
Licha ya kwamba hajawahi kusoma kabisa elimu ya sekondari kama ambavyo amekuwa akisema waziwazi katika semina na mikutano yake mbalimbali pamoja na vitabu alivyoandika, alivyopata nafasi ya kusoma chuo kikuu, aliamua kusoma kwa bidii darasani na kufuata taratibu zote za chuo hicho huku akijipunguzia baadhi ya majukumu katika makampuni yake ili aweze kuapata muda wa kutosha kujisomea.
“Kwa kweli huwa sipendi kabisa kushindwa, nilipoingia darasani mwaka 2017 kulikuwa na ushindani mkubwa, sababu wenzangu walikuwa wamesoma sekondari mpaka kidato cha sita na wengine walikuwa wana diploma, hivyo nililazimika kusoma sana ili angalau niende nao sawa, lakini juhudi zangu zimezaa matunda kwani nimekuwa mwanafunzi bora baada ya kuhitimu.
“Nimekuwa hapa chuoni kwa miaka mitatu nikisoma, hawaamini kama mimi ni darasa la saba, sijawahi kusoma elimu ya sekondari wala sijui kabisa chochote kusuhu sekondari, lakini leo nina furaha kwamba baada ya masomo yangu nimekuwa mwanafunzi baora lakini pia mbunge wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania
“Niwambie wanafunzi wenzangu mliobaki hapa shuleni na vijana wengine kote nchini, amini kwamba unaweza kuwa chochote, kikubwa ni juhudi zako tu, usikate tamaa, fanya kile unachokiamini, jitume sana utakipata kile unachokipata,” amesema Shigongo baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi.