Michuano mikubwa ngazi ya vilabu barani Afrika imewadia ambapo Tanzania bara na Visiwani imefahamu wapinzani halisi katika hatua za awali ili kusaka tiketi ya kucheza hatua ya makundi katika ligi ya mabingwa na kombe la shirikisho.
Kiungo wa Simba, Hassan Dilunga akikokota mpira katikati ya viungo wa UD Songo katika mchezo wa ligi ya mabingwa hatua ya awali ambapo mnyama aliondolewa baada ya sare ya bao 1-1.
Kwa upande wa Simba, wamepangwa kuanzia ugenini kukipiga na Plateau United ya Nigeria katika ligi ya klabu bingwa wakati Namungo wataanzia nyumbani wakipepetana na Al Rabita ya Sudan Kusini katika michuano ya kombe la shirikisho Afrika.
Uwakilishi wa vilabu kutoka Tanzania Visiwani, Mlandege itaiwakilisha nchi katika ligi ya mabingwa Afrika na imepangwa kukipiga dhidi ya CS Faxien ya Tunisia nayo KVZ itakipiga dhidi ya Al Amal ya Sudani.
Timu 68 zitashiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu na kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona, droo hiyo haikuwa na shamrashamra, wala uwakilishi wa timu na ilifanyika na kusimamiwa na kamati ya Utendaji ya CAF.
Michezo ya kwanza ya hatua ya awali itapigwa kati ya 27-29 Novemba 2020 na mechi za pili kupigwa Disemba 04-06
Timu zitakazofuzu hatua ya awali, zitatinga raundi ya kwanza ambapo watakaoshinda raundi ya kwanza watatinga hatua ya makundi wakati wale watakaoshindwa wathamishiwa hatua ya mtoano kombe la Shirikisho.
Ikumbukwe Simba ambayo msimu juzi ilipata mafanikio makubwa kwa kutinga robo fainali, lakini ilishindwa kutamba mbele ya UD Songo msimu uliopita na kuondolewa katika hatua ya awali, hivyo inahitaji kuwa makini kama watahitaji kufanya vyema kama ambavyo wamekua wakisema kila kukicha juu ya malengo ya kufanya vyema katika michuano hiyo mikubwa.